Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji hasa katika zahanati na vituo vya kutoa huduma za afya.

Mzinga aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzunduzi wa mkakati wa Shirika la WaterAid kwa kuwashirikisha wadau wa Maji na Usafi wa Mazingira (WASH).

Amesema maeneo hayo yanawakumba wanawake wengi ambao ndio watumiaji wa vituo vya afya hasa katika mambo ambayo yanahusika na uzazi.

“Tumeona kuna vituo vya afya ambavyo vinaonyesha huduma za maji na usafi wa mazingira hazijafika hili tunaliona ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa pamoja ndio maana tumeamua kuanzisha mpango mkakati wa kuonyesha maeneo ambayo tunaweza kufanya kazi ili kuwasogezea huduma za maji hasa katika vituo vya afya na shule zetu,”amesema Mzinga.

Mzinga amesema wanaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtoa mama ndoo kichwani kwa namna wanavyoona sehemu za kutoa huduma na kufikisha maji nyumbani bado haijafikia kwa asilimia 100.

Amesema kutokana na changamoto hiyo wameona athari kubwa inaenda kwa mwanamke ama kwa mtoto wa kike kutokuwepo kwa asilimia 100 ya maji na usafi wa mazingira inachangia kuwarudisha nyuma wanawake kiuchumi.

Aidha, amesema mpango mkakati huo waliouanzisha wamejipanga katika kuleta taarifa rasmi ni wapi ambapo kunahitajika kufanyiwa kazi.

Naye Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangalla, amewataka wadau wa maji na usafi wa mazingira kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa sera na mipango yake ili kuwezesha utoaji wa huduma ya maji na usafi katika jamii.

Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wanaopiga vita Usugu wa Dawa Tanzania (UVIDA) alisema licha ya Tanzania kuwa na sera na mipango mizuri, hakuna utekelezaji.

"Tuna wasomi wazuri ambao wamesoma na wamehitimu vizuri sana, wanaweka mipango vizuri lakini tunakwama kwenye utekelezaji,” amesema.

Alisema kupitia mkutano huo, wadau waazimie kuweka mikakati ya kufanikisha mipango iliyowekwa.
Awali akitoa mada katika mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Sera na Ushawishi kutoka WaterAid, Christina Mhando, alisema hadi mwaka 2021 vyanzo vinaonyesha kulikuwa na takribani vituo vya afya 8,549 zikiwemo zahanati 7,200 ambazo na asilimia 74 zinamilikiwa na serikali.

Amesema karibu nusu ya vituo hivyo havina maji ya bomba na hata vilivyounganishwa na maji ya bomba havipati maji ya uhakika.

Naye Muuguzi na Mkunga wa Kituo cha Afya cha Msanga, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Robart Mgema, alisema awali walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kituoni hali iliyowalazima wakina mama kuja na maji kwenye kituo cha afya wanapotaka kutibiwa.

Amesema kwa sasa wanashukuru kupatiwa mradi wa maji na shirika la WaterAid hali ambayo imewanufaisha wanawake kupata huduma sahihi katika mazingira bora.

“Uwepo wa mradi wa maji katika mazingira ya kutoa huduma za afya ni chanzo cha utoaji wa huduma bora yanapokopasekana maji wakina mama wanapata chanagmoto nyingi ikiwemo magonjwa ya maambukizi,”amesema.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...