Na Mwandishi Wetu,Igunga

WAZIRI wa Kilimo Husein Bashe amemtumia salamu Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina kuwa awe na shukrani kwa Serikali na kumtaka achezee sekta nyingine sio kilimo ambayo ni tegemeo kwa Taifa.

Amesema chokochoko za uongo za mbunge huyo zinapogusa sekta ya kilimo hawezi kumvumilia, kwa kuwa taifa ni kubwa mno rasiliamali ni chache hivyo jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haziwezi kurudishwa nyuma na yeye kukaa kimya.

Amesema amejipanga kwenda Kisesa na kukutana na wakulima, ili kujua mbivu na mbichi kama mbwai na iwe mbwai kwani hataki utani na uongo katika sekta hiyo inayogusa maisha ya watu.

Waziri wa Kilimo Bashe amesema hayo mara baada ya kuanza ziara ya kikazi katika wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora ambapo ameanza kwa kukutana na viongozi wa Bodi ya Pamba, Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wakulima wa Pamba.

Pia amezindua Mpango wa Kitaifa wa kuongeza Tija katika Uzalisha wa Pamba katika Kijiji cha Mbutu wilayani humo.

Amesema “Watu hawalali usiku na mchana kutafuta suluhisho kwa sekta hii, yeye alipewa nafasi alifanya nini, ni kweli haoni mabadiliko makubwa yaliyofanywa na serikali”?

“Serikali haiwezi kuwaletea wakulima wanunuzi wezi, dawa feki na mbegu feki Kisesa nakuja mtanijibu sitaki utani katika kilimo mshambulie Bashe sio hii sekta hatuwezi kuwa na taifa linatukana watu linatukana serikali tunakaa kimya”

“Watu walikuwa na mateso walikopwa, pamba zilidoda sitaruhusu mchezo wa siasa sekta ninayoisimamia, msiwe na hofu miaka miwili tumetoa ruzuku ya mbolea bure na tutaendelea kufanya hivyo na tutaendelea kununua mazao,”alisema.

Bashe amesema, “Katika shughuli za uzalishaji na uchumi mimi sifanyi siasa yeye alikuwa Waziri kwa zaidi ya miaka 20 kule Kisesa nitaenda kufanya mkutano na kuwambia wana Nzengo kuwa mbunge wemu kasema dawa za serikali feki mbegu feki na wanunuzi wanawaibia serikali.

“Tunampa nafasi alete dawa, mbegu na kununua pamba nchi yetu tumekuwa na tamaduni ya kuacha mtu anachafua serikali na hana suluhisho, naenda Kisesa tutawauliza wakulima kama yale mawazo ni ya kwao serikali tutaondoa huduma kama ni ya Mpina tutaacha….achezee sekta nyingine sio kilimo mimi nimezaliwa uswahili kama mbwai mbwai nimeamua,”alisema.

Ameongoza kuwa “Mimi ndio Waziri wa Kilimo, mimi sio wale ambao una itest serikali tena kwa uongo halafu wizara inakupigia magoti,”alisema

Waziri Bashe ametumia fursa hiyo kueleza mipango ya serikali ya kujenga mabwawa na miundombinu ya umwagiliaji ya kutosha Igunga na kuwahakikishia wananchi kuwa maji hayatageuka mateso kwa wakulima wilayani humo .

Amesema anatambua kilimo cha pamba kinavyofanya vizuri Wilayani Igunga ambapo kitakwimu ni ya kwanza au ya pili, hivyo ni lazima kuwa na uzalishaji wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya maji.

Amesisitiza kuwa, serikali imegawa trekta 500 powatila 800 kwa nchi nzima lengo ni kuimarisha sekta ya kilimo.

Aidha ili kufikia malengo hayo, ni lazima kukubaliana kuwa ni marufuku kuzalisha kwa kutegemea maoteo na atahakikisha kinajengwa kituo cha wakulima kupewa elimu, kuendelea kugawa mbegu na dawa bure kama alivyoelekeza Rais Dk. Samia.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na ana nia ya dhati ya kuinua Sekta ya Kilimo, hivyo ni wakati wa Halmashauri nchini kuwa sehemu ya kutekeleza maono hayo kwa kuinua uchumi.

“Juhudi hizi zinazofanywa na Serikali ni chachu kwa Halmashauri na Wilaya kuamka ili kusaidia kuondoa umaskini. Serikali za Wilaya na Mikoa mna wajibu wa kusimamia mabadiliko haya, tunaleta kwenu Maafisa Ugani ili waje kuwa chachu ya mabadiliko katika Sekta ya Kilimo, watumieni ipasavyo,” amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amesema Maafisa Ugani hao wahakikishe kila Kata kunakuwa na zao la uzalishaji lenye matokeo ya baadaye katika kijiji.

“Lazima tupimane kwa matokeo ya kiuchumi, katika suala la uzalishaji tusiruhusu siasa. Zao hilo ni muhimu sana katika uchumi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa,” amesisitiza Waziri Bashe.

Akitoa taarifa ya utendaji Marco Charles Mtunga, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa Wilaya ya Igunga kwa kuwa inazalisha zao la Pamba kwa kiasi cha takribani tani 22,000 hadi 26,000.

Ameongeza kuwa hatua ya Wilaya hiyo kuwezeshwa zana bora za kilimo, mafunzo na kupatiwa Maofisa Ugani itakuwa na uwezo wa kuzalisha hadi tani 100,000 ambapo kwa kila mkulima ni wastani wa uzalishaji ni kilo 300 (ambayo ni tani 0.3).

Kwa sasa, zao la Pamba nchini linazalishwa kwa tani 284,000 ambapo malengo ya nchi ni kuwa na uzalishaji wa tani 500,000.

Mkutano huo wa awali, ulihudhuriwa pia na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Cornel Magembe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge na Mkuu wa Wilaya wa Igunga, Mhe. Sauda Mtondoke.

Aidha Cornel Magembe, amesema Mkoa wa Tabora upo salama na wanamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kupata msaidizi wa kweli wa Wizara ya Kilimo.

“Zao la pamba ndiyo limetufikisha hapa, uchumi wa Mkoa unategemea zaidi zao hilo na tunayo nafasi ya kurudisha zao la pamba kwa kufanya Kilimo cha kibiashara,” amesema Magembe.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...