Na Mwandishi Wetu

Halmashauri ya Jiji la Tanga imefungua dirisha la utoaji mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani Kwa kina mama, vijana na watu wenye ulemavu, kuanzia leo tarehe 29 Septemba 2024, na litakuwa wazi kwa mwezi mmoja, na kufungwa Oktoba 29 ambapo Serikali imefanya maboresho ya sheria na kanuni za mikopo hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Mhandisi Juma Hamsini, alisema Halmashauri imeidhinisha kiasi cha zaidi ya shilingi Billion 3, ambapo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanachagua biashara yenye manufaa na si kuiga biashara ambazo hawana elimu nazo, huku akitoa wito kwa maofisa mikopo kujiepusha na undugu, na kufuata kanuni zilizowekwa na Serikali.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga Simon Mndende amesema kuwa matarajio yao kwa Halmashauri nikuhakikisha wanakopesha vikundi visivyopungua 135 ndani ya kata 27 zilizopo Jijini humo.

Mndende amesema kwa marekebisho ya sheria yaliofanyika kikundi ndio dhamana ya mkopo, japo kila mwanakikundi ana uhuru wa kufanya biashara tofauti ndani ya kikundi.

Aprili, 2023 serikali ilisitisha utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani nchi nzima kutokana na changamoto mbalimbali kama vile vikundi kutorejesha mikopo kwa wakati.

Baada ya hapo serikali iliunda timu ya kuandaa maboresho ya utoaji na usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mapendekezo yaliyotolewa na timu iliyoundwa yamepelekea kuandaliwa Kanuni mpya za utoaji na usimamizi wa mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2024.

Pamoja na mambo mengine, kanuni mpya zimeongeza sifa ya umri wa vijana kutoka miaka 18 - 35 ya awali na kuwa miaka 18 - 45.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...