NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MSIMAMIZI wa Uchaguzi katika halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Shadrack Mhagama amevitangaza vijiji 157 na Vitongoji 699 katika halmashauri hiyo kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.
Mhagama ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo aliyasema hayo katika kikao chake na Watendaji wa Kata, Vijiji na Vitongoji pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa kwa lengo la kutangaza majina na mipaka ya vijiji na vitongoji katika halmashauri hiyo.
Alisema kuwa, wameainisha mipaka ya kila kata, na mipaka ya kila kijiji na kitongoji ambapo maeneo hayo ndiyo yatakayohusika katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo halmashauri hiyo inakata 32 na vijiji 157 na vitongoji 699.
Mhagama alisema kuwa, kwa sasa wanaendelea na maandalizi mbalimbali ya kuelekea uchaguzi huo ambapo amewataka Watendaji wa kata, vijiji na vitongoji kubandika makaratasi hayo yanayoonyesha mipaka katika maeneo mbalimbali ili wananchi watambue mipaka.
”Wapo wananchi ambao walikuwa hawaamini kama maeneo yao hayapo katika halmashauri ya Moshi ambayo ni maeneo mawili ya kata ya Kimochi ambacho ni kijiji cha Mdawi na kijiji cha Kikarara wao walikuwa wanaamini wapo Manispaa ya Moshi ukweli ni kwamba wapo halmashauri ya Moshi na mipaka hiyo haijabadilishwa” alisema Mhagama.
Alisema kuwa, majina ya vijiji hivyo na vitongoji vyake na anayewatambua ni halmashauri ya wilaya ya Moshi na kuwataka kujipanga kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Aidha Msimamizi huyo wa uchaguzi amewaomba wananchi kujitokeza kujiandikisha tayari kwa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo zoezi hilo litaanza Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu ambapo wamejipanga kuwafikia wananchi wote.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi kuendelea kuwa na amani na utulivu ili kuweza kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa na kudai kuwa mpaka sasa hawana changamoto yoyote na wamejipanga kukutana na wadau mbalimbali na kuzungumza nao ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaenda kwa amani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...