Na Raisa Said, Tanga

Maajabu Maingwa (25), mkazi wa kijiji cha Tunguli, wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, ana kila sababu ya kufurahi. Miaka mitatu iliyopita alipoteza mtoto wake aliyezaliwa njiti kutokana na ukosefu wa huduma maalum katika hospitali ya wilaya. Lakini mwezi uliopita, alifanikiwa kumzaa tena mtoto njiti na safari hii mtoto wake yuko hai, akipatiwa matunzo sahihi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo.

"Nashukuru kwa huduma hizi mpya. Sasa mtoto wangu anaendelea vizuri na nashikilia matumaini mapya," alisema Maingwa kwa furaha.

Mwanamvua Ramadhani, mkazi wa Donge, Jiji la Tanga, pia anashuhudia maboresho hayo. "Huduma hizi zimeanza kupatikana katika baadhi ya vituo vya afya jijini Tanga , hospitali mpya ya wilaya na Bombo. Watoto wengi sasa wataishi," alisema.


Takwimu za Watoto Njiti

Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya watoto njiti, ambapo takriban asilimia 10 ya watoto huzaliwa kabla ya wakati. Hii inamaanisha zaidi ya watoto 200,000 wanazaliwa njiti kila mwaka nchini. Mkoa wa Tanga unakabiliwa na sehemu kubwa ya tatizo hili, ukiripoti takriban watoto 1,000 hadi 1,200 wanaozaliwa njiti kila mwaka.

Kutokana na idadi hiyo kubwa, hitaji la kuboresha huduma za utunzaji wa watoto wachanga ni muhimu kwa kupunguza vifo na kuboresha afya ya watoto wachanga walio katika mazingira hatarishi.

Maboresho Makubwa Hospitali ya Bombo

Huduma za watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo, zimepiga hatua kubwa. Kuanzia mwaka 2017, wodi ya watoto njiti imepanuliwa kutoka chumba kidogo cha kuhudumia watoto wanane hadi wodi kamili yenye vifaa vya kisasa.

Dk. Salehe Mohamed, Daktari Bingwa wa Watoto katika hospitali hiyo, anasema, “Uwekezaji wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umetuwezesha kuboresha huduma hizi. Tumepata vifaa vya kisasa kama vile mashine za joto na CPAP kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya kupumua, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia vifo vya watoto wachanga hapo awali.”

Maendeleo hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita , sambamba na kuungwa mkono na wadau mbalimbali ikiwemo makala na vipindivya redio vilivyofanywa kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendelo ya Mtoto (PJT MMAM) ambavyo vilisababisha Mamlaka ya Bandari ambayo ilitoa vifaa kwa ajili ya huduma ya watoto njiti katika Hospitali hiyo mwaka 2020.

Huduma hizi sasa zinakidhi mahitaji ya watoto wachanga kutoka wilaya zote tisa za Mkoa wa Tanga, na zimesaidia kuokoa maisha ya watoto wengi.

Wodi Yenye Vifaa Maalum

Wodi ya watoto wachanga sasa ina maeneo manne: Ofisi za Madaktari, Huduma ya Kangaroo (kuweka watoto njiti karibu na miili ya wazazi kwa ajili ya joto), wodi ya watoto wachanga, na Kitengo cha Utunzaji wa Watoto Wenye Hali Mbaya. Wodi hiyo imewekwa incubators na vifaa vya kisasa vya kusaidia watoto wachanga kuishi.

Dk. Mohamed anaeleza kuwa huduma hii ni msaada mkubwa kwa watoto wengi wanaozaliwa na homa ya manjano. “Tunatumia mashine za phototherapy kutibu homa ya manjano, na ni muhimu kuelewa kwamba mwanga wa jua pekee hauwezi kutibu tatizo hili ipasavyo,” alisema.

Changamoto Zinazoendelea

Licha ya maboresho hayo, Dk. Mohamed anasisitiza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa zaidi kutokana na ongezeko la watoto wanaozaliwa njiti. Pia aliweka msisitizo juu ya umuhimu wa elimu kwa wazazi na jamii ili kuhakikisha huduma bora na uangalizi kwa watoto hawa.


Hatua Zaidi Zinazotarajiwa

Katika Wilaya ya Handeni, Mganga Mkuu Dk. Kisaka Kachua amesema kuwa hospitali mpya ya halmashauri inatarajia kuanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya watoto wachanga. Kitengo hicho kimeshaandaliwa, na vifaa vimeagizwa.

Naye Mkurugenzi wa shirika la United Help for Tanzania Children (UHTC), Dk Regis Temba amesema kuongezeka kwa vifaa vya kusaidia watoto njit imepelekea vifo kwa watoto wa namna hiyo kupungua.

Dk Temba ambaye shirika lake ndilo linaratibu Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendelo ya Mtoto (PJT MMAM) mkoani Tanga kwa kushirikiana na serikali ya mkoa waTanga amesema kwa kiasi kikubwa wauguzi wameweza kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na ufanisi wa hali ya juu

hivi karibuni ,Waziri wa Afya Jenista Mhagama alisisitiza dhamira ya serikali ya kulinda maisha ya watoto wachanga kabla ya wakati, akitangaza mipango ya kusambaza vifaa vya matibabu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya Continuous Positive Airway Pressure (CPAP) kwa hospitali zilizo na wodi maalum za watoto wachanga.

Waziri Mhagama alitoa taarifa hiyo wakati akitoa vifaa tiba baada ya kutembelea Bohari ya Dawa (MSD).

Vifaa hivyo 130 vyenye thamani ya 212.8M/ vilinunuliwa na MSD ili kutekeleza agizo la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan lililolenga kupunguza vifo vya watoto wachanga.

“Tuendelee kusambaza mashine hizi ili ziweze kupatikana katika vituo vyote vya afya na hospitali za wilaya, ni vyema tukahakikisha kila kituo kina mashine zisizopungua tano, kwani tunaweza kukutana na watoto wengi wanaozaliwa kabla ya wakati kwa wakati mmoja.

Ni lazima tuwasaidie watoto hawa wachanga ili wasipoteze maisha,” alisisitiza Waziri.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...