NA WILLIUM PAUL, DODOMA.
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais na Serikali za mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Zainab Kasimba amesema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya Elimu na itaendelea kuboresha mazingira mazuri ya walimu kufundishia.
Naibu Waziri Zainab alitoa kauli hiyo alipokutana na Walimu Wakuu na Makamu wao wa shule za Sekondari zilizopo Jimbo la Same mashariki Bungeni jijini Dodoma kwa mwaliko wa Mbunge wa Jimbo hilo Anne Kilango Malecela.
Alisema kuwa, kwa sasa serikali imeanza kujikita katika ujenzi wa nyumba za Walimu ili kuhakikisha kuwa wanaishi karibu na maeneo yao ya kazi na kuwataka kufanya kazi kwa kujitoa na uzalendo mkubwa kwani Taifa linawategemea.
"Kazi ya Walimu ni kazi inayotegemewa na Taifa hivyo serikali itaendelea kuboresha sekta ya Elimu ili walimu mfanye kazi katika mazingira mazuri na rafiki kwenu na niwaombe muendelee kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kutimiza maono yake aliyoyaanzisha katika sekta ya Elimu" Alisema Zainab.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu kutoka Wizara ya Tamisemi, Dkt. Seleman Emmanuel alisema kuwa, kwa sasa serikali imeshaanza kulipa madai yote ya walimu pamoja na kuwapandisha madaraja.
Dkt. Emmanuel aliwataka walimu kufanya kazi kwa bidii huku wakitambua kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali na kuwathamini mchango wao mkubwa katika Jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Walimu wenzake, Mwenyekiti wa Wakuu wa shule Jimbo la Same mashariki, Emmanuel Malya ambaye Mkuu wa shule ya sekondari Bemko, alisema kuwa, kwa sasa sekta ya Elimu haina deni na serikali kwani imefanya mambo makubwa katika sekta hiyo.
Malya alisema kuwa, wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiibeza serikali kwa kutotambua imefanya nini na kudai kuwa sasa imefika wakati ambapo walimu wanapaswa kuwaelimisha wananchi na kuwaeleza waziwazi yaliyofanywa na serikali.
"Serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha miradi mingi inatekelezwa hasa kwenye sekta yetu ya Elimu sasa sisi walimu tunadhamana ya kwenda katika jamii na kutoa Elimu na kuisemea miradi hiyo" Alisema Malya.
Aidha Mwenyekiti huyo aliipongeza serikali kwa kusikiliza kilio chao cha upandishwaji madaraja pamoja na ulipaji wa madai yao ya malimbikizo ya mshahara pamoja na madai ya fedha za likizo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela alitumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kwa kuanzisha shule mpya za Sekondari tatu katika Jimbo hilo huku akidai kuwa Jimbo hilo pia limepokea fedha nyingi katika sekta ya Elimu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...