Na MWANDISHI WETU

WADAU wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wameiomba Serikali kupatia suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani barabara ya Serengeti

Akizungumza leo na waandishi wa habari ambao wametembelea eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TANAPA katika kuboresha barabara hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiriwa na wingi wa magari wastani wa magari 600 kwa siku.

Macha aliyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika barabara ya Naabi hadi Seronera.

Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.

“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili magari ni mengi sana na ndio chanzo kikuu cha ukorofi wa barabara hii”

“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” alisema Macha

Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika ili kupunguza adha hiyo kwa wageni

“Shirika limeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.

Aidha, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara katika hifadhi za Taifa zote nchini.

Pia, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA inafanya jitihada za haraka kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi zote za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na idadi ya magari yanayotumia barabara hiyo.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephen Msumi alisema kuwa menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika hifadhi ikiwemo kudhibiti mwendokasi pamoja na kuzingatia alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayojitokeza kwa kutozingatia sheria hizo.

Hifadhi ya Taifa Serengeti inafanya ukarabati wa barabara zake ili kuondoa adha hiyo na kuzifanya barabara zote ndani Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...