SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania ( TANAPA) limezindua rasmi msimu wa nne wa kampeni ya Twendezetu kileleni 2024, ili kuhamasisha Watanzania kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 6, 2024, jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Lyimo, amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha utalii wa ndani na kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa kuangazia hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
“Tunafahamu kuwa kila ifikapo Desemba 9, nchi yetu huadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika. Kama TANAPA, tumekuwa tukitumia siku hii kutangaza utalii wa hifadhi ya taifa ya Mlima Kilimanjaro, na tunawahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupanda mlima huu maarufu," amesema Lyimo.
Kamishna Lyimo amesem utamaduni wa kupanda Mlima Kilimanjaro ulianza mwaka 1961 wakati Tanganyika ilipopata uhuru, ambapo Kapteni wa Jeshi la Wananchi, Alexander Nyirenda, alipandisha Mwenge wa Uhuru kileleni mwa mlima huo.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu TANAPA, Mapinduzi Mdesa, amesema kuwa Mlima Kilimanjaro una vivutio vingi kama vile maporomoko ya maji, vinavyovutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa katika msimu huu, shughuli mbalimbali za kiutalii kama vile upandaji wa parachute, mbio za baiskeli, na michezo kama mpira wa miguu zitaendelea kufanyika.
Pia Mdesa amesema kuwa katika maadhimisho hayo, kutakuwa na njia tatu rasmi za kupanda mlima – Marangu, Machame, na Lemosho – ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni "Stawisha Uoto wa Asili Tanzania, Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro."
Kwa upande wa Wawakilishi wa Makampuni ya kuongoza Watalii kupanda Mlima Kilimanjaro wamesema wapo tayari kutoa huduma bora kwa wananchi ambao watajitokeza kupanda mlima hivyo wamewasihi wananchi kujitokeza kupanda mlima ikiwa ni kufanya utalii wa ndani.
Muongoza wageni kutoka kampuni ya utalii ya ZARA, Faustin Chombo, ameishukuru serikali kwa msaada wake wa kuhamasisha utalii wa ndani.
Ameeleza kuwa mwaka jana walifanikiwa kupata watalii 200 waliopanda mlima huo kupitia kampeni ya Twenzetu Kileleni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...