Na Ashrack Miraji Lushoto Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Buriani ameagiza Tamasha la Utalii la Usambara 2024 (Usambara Tourism Festival 2024) litumike kuhamasisha Wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Amesema hayo alipotembelea Wilayani Lushoto akiwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa kwa ajili ya kukagua maandalizi ya Tamasha hilo kubwa linalotarajiwa kufanyika Septemba 21-22, 2024 katika viwanja vya Nyerere Square.
Mhe. Dkt. Batilda alisema kwamba kwa sababu Tamasha hilo litahudhuriwa na watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Lushoto pamoja na Tanzania kwa ujumla, hivyo ni sehemu sahihi kabisa kuhamasisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
"Kama mnavyojua kuwa kwa sasa Taifa letu liko kwenye maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Jana 16/09/2024 Mhe. Waziri wa TAMISEMI (Mhe. Mohamed Mchengerwa), alitangaza Maeneo ya Utawala na Mipaka ya nchi nzima na mimi (Dkt. Batilda) nikatangaza kwa Mkoa wa Tanga." Alisema Dkt. Batilda.
"Hivyo Tamasha hili ni 'platform' (Jukwaa) nzuri ya kuwafukia watu wengi zaidi kuwahamasisha na kuwaelimisha juu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwenye mabango na matangazo yote tukumbuke kuweka kauli mbiu (Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi) ya uchaguzi huu." Aliendelea kusema Dkt. Batilda.
Katika hatua nyingine Dkt. Batilda alipokea taarifa ya maandalizi ya Tamasha la Utalii la Usambara 2024, kutoka kwa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Dkt. batilda alikagua maandalizi ya tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Septemba 21-22, 2024, huku Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...