Na. Valeria Adam, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aeleza faida za nishati safi kwa matumizi ya kupikia na kuwataka wananchi wa Dodoma kuacha kutumia nishati chafu kwa matumizi ya nyumbani na sehemu za kazi.
Aliyasema hayo katika halfa ya ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko 1,000 kwa shule, zahanati, vituo vya afya, vituo vya makao ya watoto na mama na baba lishe huku akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia, kuboresha afya za watumiaji na kulinda mazingira.
Alisema kuwa nishati safi ina faida kubwa kwa watumiaji na mazingira hatua hiyo inalenga kuimarisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia, kuboresha afya za watumiaji, na kulinda mazingira. “Faida za nishati safi ni pamoja na matumizi bila kuathiri afya za watumiaji. Pia, itapelekea hewa ya oksijeni kuongezeka na miti kuendelea kukua, na hivyo, Dodoma itaendelea kuwa salama” alisema Senyamule.
Aliongeza kuwa biashara ya nishati safi ina fursa kubwa kwa sasa kwasababu watumiaji watazidi kuongezeka, na watu wataendelea kununua gesi mara baada ya mitungi yao kuisha. “Nishati safi ni biashara kubwa kwa sababu watumiaji watazidi kuongezeka, lakini pia watakapomaliza gesi wataendelea kuijaza mitungi, na hivyo matumizi ya gesi hayataisha” alisisitiza Senyamule.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa anatamani kuona halmashauri inajumuisha kifungu maalum kwenye bajeti yake ambacho kitaruhusu taasisi hizo kununua gesi kila mwezi. “Matarajio yangu kwenye bajeti ya halmashauri itaongeza kifungu mtakachotenga fedha kila mwezi kwa shule na vituo vya afya viwe na uwezeshaji wa kununua gesi na kujaza kwenye mitungi” alisema kwa msisitizo Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, alisema kuwa matumizi ya nishati safi yanachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira. “Kwa miaka ya hivi karibuni, ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira umepungua sana na kaulimbiu yetu ya 'Kukijanisha Dodoma' imeanza kuzaa matunda. Sasa, ukijani tumeanza kuuona katika maeneo yetu” alisema Mavunde.
Pia, aliahidi kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati mbadala, pamoja na aina ya mkaa usio na madhara kwa mazingira, kama ule wa kutumia makaratasi, plastiki, na magome ya miti. “Sisi kama viongozi ni lazima tuwatoe wananchi wetu kwenye kukata miti kutengenezea kuni na mkaa na kuwahamasisha kuacha kutumia mkaa na badala yake kutumia nishati safi” aliongeza Mavunde.
Hatua ya kugawa mitungi ya gesi na majiko inaonesha dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi kwa faida ya afya zao na mazingira huku ikikuza uchumi wa taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...