Mazoezi ya mchezo yakiendelea katika msitu wa Pande Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mchezo mpya wa Adventure Racing unaoendelea katika msitu wa Pande ,jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa Adventure Racing washiriki wakiwa katika mazoezi katika msitu wa Pande
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WATANZANIA wametakiwa kushiriki mchezo mpya wa kimataifa wa kupitia vikwazo (World Obstacle Adventure Racing) unaoanzishwa hapa nchini ili kupata fursa za kuiwakilisha nchi katika michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo michezo maarufu ya Olimpiki.
Mchezo huu umekuwa ukijipatia umaarufu duniani ikiwemo katika bara la Ulaya ambapo kuna michuano mbalimbali inafanyika.
Akiongea wakati wa mafunzo ya vitendo yanayoendelea katika Mbuga ya Pande (Pande Game Reserve) iliyopo Dar es Salaam, Mratibu Abdallah Chapa amesema mchezo huu unajizolea umaarufu na ni moja ya michezo shindani katika michuano ya Olimpiki.
Hivyo amewataka wanamichezo wa michezo mbalimbali wakiwemo wa riadha kujitokeza kwa wingi na kujiunga kwa sababu mchezo huu unajumuisha michezo mbalimbali ikiwemo kukimbia mbugani, kutambaa chini ya nyavu, kupanda mti kwa kutumia kamba na michezo mingine mbalimbali yenye kufurahisha.
Moja ya vikwazo pendwa ya mchezo huu inayoonekana katika televisheni ni mchezaji kuparamia juu ya miti au bomba maalumu na kuvuka eneo ambalo akishindwa anaaungukia chini ya maji.
Amesema Tanzania kuna wachezaji wenye vipaji ambao wana nafasi nzuri ya kujifunza sheria na taratibu za mchezo huu na kufanya vizuri.
“Tuna fursa za kupata medali kupitia mchezo huu na ndio maana tunatoa mafunzo kwa walimu wajue sheria na taratibu ili waweze kufundisha wachezaji watakaotuwakilisha vyema katika michuano mbalimbali ya kimataifa,” amesema Chapa.
Amewashukuru wadhamini Well Mark Legal, Kilimanjaro Fresh, The Green Sports Park, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori ( Tawa) na Adventure Races kwa kufanikisha mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki hao, Mkenya Ian Ochieng, ambaye ni mwalimu wa viungo amesema mchezo huu utazisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuongeza nafasi ya kupata medali katika michuano ya Olimpiki na kutoa wito wa kufanyika maadalizi ya kutosha kwa wanamichezo.
Zaidi ya wanamichezo 50 kutoka michezo mbalimbali ikiwemo riadha na mpira wa kikapu wanashiriki kozi ya darasani na vitendo ya ukocha ya Level 1 inayoendeshwa na mkufunzi Nayibe Statia kutoka visiwa vya Carribean.
Washiriki hao walishiriki michezo mbalimbali katika mbuga ya Pande iliyopo Mabwepande ukiwemo wa riadha, kupanda juu ya mti kwa kutumia kamba na kuruka uzio.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...