Wananchi kote Nchini wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kuimarisha afya zao sambamba na kutunza mazingira.

Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2024 Wilayani Bukombe Mkoani Geita na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage wakati wa Semina maalum ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wakazi wa Wilaya hiyo.

"Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, anatupenda na anafanya kila njia kuhakikisha kila mwananchi anapata bidhaa za Nishati Safi za kupikia kwa gharama nafuu", alisema Mhandisi Mwijage.

Mgeni rasmi katika Semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Muragili alimshukuru Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku katika bidhaa za Nishati Safi za Kupikia suala ambalo alisema linakwenda kuimarisha afya za wananchi sanjari na kuhifadhi mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa alisema yameathiriwa na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

"Leo ni siku ya kihistoria kwa wakazi wa Bukombe, tunakwenda kupokea mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku na hizi ni jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza," alisema Muragili.

Aliwasihi wananchi wote watakaojipatia mitungi hiyo kuhakikisha inapomalizika wanajaza ili kuendelea kutumia Nishati Safi ya Kupikia na si kurejea katika matumizi ya kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa Semina hiyo, Mhandisi Mwijage alisema Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha bidhaa za Nishati Safi za Kupikia zinafika katika kila pembe ya nchi ili kumuwezesha kila mwananchi kuachana na matumizi ya Nishati isiyo safi na salama.

"Serikali kupitia REA imetoa ruzuku kwa bidhaa za Nishati Safi za kupikia ili kuhakikisha hakuna mwananchi anaachwa nyuma," alisema.

Mhandisi Advera alisema kwa bidhaa za mitungi ya gesi (LPG), Serikali imeingia makubaliano na watoa huduma ya kusambaza mitungi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ambapo katika kila Wilaya kiasi cha mitungi 3,255 itasambazwa.

"Kwa hapa Bukombe, mtoa huduma atakayesambaza mitungi ni Kampuni ya Manjis ambapo mitungi hii ya kilo sita ikiwa kamili na vichomeo vyake itatolewa kwa shilingi 17,500 tu ambayo ni sawa na nusu bei," alisema Mhandisi Mwijage.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Yusuph Yusuph alipongeza REA kwa kutekeleza dhamira ya Rais Samia kwa vitendo na alisema semina hiyo itaongeza uelewa miongoni mwa wananchi kuhusiana na suala zima la nishati safi za kupikia sambamba na kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu za kupikia.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...