EFTA yafadhili wakulima Watano Kutembelea Uturuki Kujifunza Kilimo: Safari ya Kubadilishana Maarifa na Ubunifu wa Kilimo
Na Magesa
Magesa
Octoba, 2024.
Dar es Salaam.
Katika juhudi
za kuhakikisha wakulima nchini wanapata maarifa na mafunzo
zaidi ya mbinu bora za kilimo.
Kampuni ya
EFTA inayojishughulisha na utoaji wa mikopo ya mashine za aina mbalimbali kwa
wakulima bila dhamana imefadhili wakulima watano kutoka maeneo mbalimbali
nchini kutembelea nchini Uturuki kwa lengo la kujifunza zaidi mbinu bora za
kilimo ambazo wakulima wa Uturuki wamekuwa wakizitumia katika kujihakikishia
kilimo chenye tija.
Akizungumza
kuhusu ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA Bwana Nicomed Bohay, amesema
ziara hiyo nimatokeo ya promosheni ya “Nunua Trekta Ushinde Safari ya
Uturuki" iliyozinduliwa mwezi machi, 2023 ikiwa na lengo la
kuwahamasisha wakulima nchini kujitokeza kwa wingi na kukopa Matrekta aina ya
New Holland TT75 4WD ambayo kampuni ya EFTA iliyanunua kutoka kwa kampuni ya
CNH Industrial ya nchini Uturuki ambao ndio watengenezaji wa Trekta za New
Holland Pamoja na zana zingine za kilimo za chapa New Holland.
Akifafanua
zaidi kuhusu kampeni hiyo, Bohay, amebainisha kuwa Lengo kuu la kampeni hiyo
lilikuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa matrekta ya New Holland TT75 4WD
yanapatikana kwa urahisi nchini pindi wakulima wanapoyahitaji.
“Miaka ya
nyuma ilimuhitaji mkulima kusubiri siku sitini hadi tisini kupata Trekta
analohitaji ili lisafilishwe kutoka uturuki mpaka limfikie, na hii kwa kweli
ilikuwa changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu na hasa ukizingatia wao hutegemea
misimu ya mvua kufanya shughuli za kilimo” alisema Bohay
Kwa kuuona
ukubwa wa changamoto hiyo kampuni yetu iliamua kununua Trekta zaidi ya 200 aina
ya New Holland TT75 4WD na kuzileta hapa nchini ili pindi wakulima wanapokuwa
wanazihitaji basi waweze kuzipata ndani ya muda mfupi. Aliongeza Bohay
Bohay amesema
kuchochea mwitiko wa wakulima kununua au kukopa Trekta hizo kwa wingi ambazo
zilikuwa zikipatikana kwa urahisi nchini ndio maana walikuja na wazo la Promosheni
hiyo ambayo Pamoja na malengo yake ya msingi ililenga kuwawezesha wakulima
watakaoibuka washindi kujipatia nafasi ya kutembelea Kiwanda cha Matrekta cha
New Holland nchini Uturuki Pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali ambazo
wakulima wa Uturuki huzitumia kujipatia mazao mengi zaidi.
Katika
kipindi cha siku nne za ziara , wakulima hawa walitembelea kiwanda cha
utengenezaji wa Matrekta cha New Holland nchini Uturuki, ambapo waliona
mchakato wa kutengeneza matrekta ambayo kwa sehemu kubwa hutumiwa na wakulima
wa Tanzania. Ziara hii iliwapa uelewa wa kina kuhusu teknolojia na uhandisi
unaohusika katika kuunda Matrekta hayo Pamoja na mashine zingine.
Ziara hiyo
pia ilihusisha warsha na semina, ambapo wakulima walijifunza ubunifu mbalimbali
katika kilimo endelevu, kilimo hai, na matumizi ya zana za kidijitali katika
kilimo cha kisasa.
Kwa upande
wake kiongozi wa msafara huo, Bw. Clerius Asiel, Mkuu wa Idara ya Mauzo na
Masoko wa EFTA, amesema safari hiyo imekuwa ni fursa muhimu sana kwa wakulima
alioambatana nao kujifunza zaidi mbinu bora za kilimo
“Wakulima
hawa tayari wanatumia mbinu za kisasa za kilimo, lakini kutokana na maendeleo
ya haraka ya teknolojia, kuna mengi zaidi ya kujifunza. Ziara hii imewaruhusu
kufikiria nje ya mbinu walizokuwa wakitumia na kuchunguza jinsi wanavyoweza
kutumia mbinu za kisasa zaidi ili kuongeza mavuno yao.” Amesema Clerius
Kwa upande
wao baadhi ya washindi wa ziara hiyo wameishukuru sana kampuni ya EFTA kwa
fursa hiyo ya ziara ya mafunzo nchini Uturuki maana wamejifunza mengi ambayo
wameahidi kuyatumia katika kuleta mapinduzi katika shughuli zao za kila siku za
kilimo.
Peter Keppa ni
mmoja wa Washindi wa ziara hiyo akitokea wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara, anasema
ziara hiyo imemtoa “tongotongo” “ Mwanzoni nilijua kwa kumiliki tu Trekta basi
tayari unakuwa mkulima wa kisasa, ila ukweli sikuwa sahihi baada ya ziara hii
na maarifa niliyoyapata na huku kwa wenzetu sasa ndio naenda kuwa mkulima wa
kisasa maana nimekusudia elimu yote niliyoipata huku kuitumia kwa usahihi”
Amesema Keppa
Kupitia ziara
hiyo Keppa amesema wakulima wa Uturuki hawategemei mvua kupata mavuno, “sehemu
kubwa ya kilimo chao ni cha umwagiliaji, nadhani huku ndiko hata sisi wakulima
wa Tanzania Tunatakiwa tuelekeze mawazo yetu sasa, wenzetu mvua sio changamoto
kwao, kwa sababu wamewekeza sana katika mifumo ya umwagiliaji, ambayo
inahakikisha mavuno yao yapo salama muda wote.”
Kwa upande
wake Bwana, Nobert Alexander mshindi mwingine aliyepata Bahati ya kuwa kushinda
fursa ya kuwa katika ziara hiyo amewashukuru sana kampuni ya EFTA na kuelezea
furaha yake kwa maarifa aliyoyapata katika ziara hiyo.
“Ziara hii
imetupa maarifa ambayo hatukuwa nayo kabla. Tumeona jinsi teknolojia ya kisasa
inaweza kurahisisha kilimo, na ninatarajia kutumia yale niliyoyajifunza ili
kuongeza mavuno yangu, lakini pia nitawashirikisha pia na wakulima wenzangu ili
sote kwa Pamoja tufanikiwe.” Amesema Nobert
Mkulima
mwingine, Bw. Charles Gidamoni, aliongeza, “Hii ilikuwa ni uzoefu wa
kubadilisha maisha. Ujuzi tuliopewa hautabadilisha tu mashamba yetu, bali pia
utakuwa mwongozo kwa wakulima wengine katika jamii zetu.”
Kupitia ziara
hii wakulima hawa sasa wanao uhakika wa kuboresha kilimo chao kwa kutumia
teknolojia mbalimbali za kilimo huku wakiwa na uhakika wa kupata mikopo ya
mashine za kilimo watakazo zihitaji ili kutoka EFTA bila dhamana ili kuongeza
ufanisi katika kilimo chao.
Washindi wa Nunua Trekta Ushinde Safari YaUturuki wakiwa katika Uwanja wa ndege wa Istanibul mara baada ya kuwasili nchini Uturukitayari wa ziara ya Mafunzo ya Kilimo.
Picha za matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Picha za matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Picha za matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...