Na Lilian Lundo - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuna sababu ya ziada za kuandika historia ya Sokoine ikiwa ni miaka 40 tangu atangulie mbele za haki.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo Septemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizindua kitabu cha maisha na uongozi wa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Moringe Sokoine.

“Kitabu hiki kimeweka kumbukumbu ya kina ya maisha na uongozi wa Sokoine, kimewezesha ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wenzake kutoa ushuhuda mwingi kuhusu alivyoishi na pia kimetambua mchango wake kwenye ujenzi wa taifa letu,” amesema Mhe. Rais.

Ameendelea kusema kuwa, mapito ya taifa huchukuliwa kwa mitazamo na tafsiri tofauti tofauti, kwa kuangalia historia ya nchi. Aidha, kupitia maisha ya Sokoine, tunapata uelewa na picha kamili zaidi. Hivyo kuna sababu ya ziada za kuandika historia ya Sokoine ikiwa ni miaka 40 tangu atangulie mbele za haki.

“Tunapoandika tunapata pia fursa ya kuangalia mapito ya nchi yetu kwa undani zaidi, kama ambavyo kitabu hiki kimefanya kuhusu Vita vya Kagera dhidi ya mvamizi Nduli Idi Amin, na katika simulizi nyingine nyingi kwenye kitabu,” amefafanua Mhe. Rais

Aidha amesema kuwa, kitabu hicho hakiandiki historia mpya kuhusu Sokoine, kwani Sokoine alijiandikia historia yeye mwenyewe. Hivyo kitabu hicho kinajaribu kuweka pamoja mapito ya kiongozi huyo wakati akijiandikia historia yake.

“Kupitia kitabu hiki, tunapata fursa ya kumfahamu Sokoine kupitia maisha yake binafsi tangu alipozaliwa hadi kushika madaraka makubwa ya uongozi nchini, akiwa kama kijana wa Kimasai aliyedumisha na kuheshimu tamaduni na mila za jamii yake,” amefafanua Mhe. Rais.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango amemuomba Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha viongozi wastaafu, fedha na rasimali watu, ili waandike tawasifu zao wakiwa hai.

“Uandishi wa tawasifu baada ya kiongozi kufariki, ni mgumu sana, na unatokana na ukweli kwamba, baadhi ya taarifa binafsi zisizoandikwa sio rahisi wengine kuzifahamu. Kwa hiyo Mhe. Rais, ninawaomba viongozi ambao Mungu amewaruzuku uhai hadi sasa , wajitahidi kuandika kitabu cha tawasifu wangali hai,” amesema Mhe. Dkt. Mpango.

“Mhe. Rais ninaomba serikali yako ione uwezakano wa kuwawezesha viongozi wetu wastaafu, fedha na rasimali watu, ili waweze kufanya kazi ya kuandika tawasifu zao,” amesema Dkt. Mpango

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 mpaka 1980 na 1983 mpaka 1984 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo tarehe 30 Septemba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 mpaka 1980 na 1983 mpaka 1984 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), kushoto ni Balozi Joseph Sokoine mtoto wa Hayati Sokoine leo tarehe 30 Septemba, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Familia ya hayati Edward Moringe Sokoine kabla ya kuzindua Kitabu kinachohusu Maisha na Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo tarehe 30 Septemba, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Familia ya hayati Edward Moringe Sokoine mara baada ya kuzindua Kitabu kinachohusu Maisha na Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo tarehe 30 Septemba, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali mara baada ya kuzindua Kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine kinachohusu Maisha na Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo tarehe 30 Septemba, 2024.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...