Na Linda Akyoo -Same.
Wananchi wa Kata ya Kihurio Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 4.17 ambao utaenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 10,000 wa Kata hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba na kumtambulisha mkandarasi wa mradi, Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe.Kasilda Mgeni amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa viwango vya utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kuzingatia mkataba unavyomtaka, ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji wanayokabiliana nayo wananchi wa kata ya Kihurio kwa sasa.
Hata hivyo DC Kasilda amewasitiza Wananchi wa Kihurio kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Mkandarasi kwenye kipindi chote cha utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa kwanza wa mitambo itakayotumiwa na wakandarasi kutekeleza mradi huo.
“Mradi huu umekuja wakati sahihi kwa watu sahihi, niwatake Wananchi wenzangu wa Kihurio kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na kuwa mstali wa mbele katika kulinda na kutunza miundombinu itakayotumika kwenye mradi” alisisitiza Mhe Mgeni
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Abdallah Gendaeka amesema, mradi utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia tarehe Desemba 2024 hadi Desemba 2026. Kazi hiyo itakayofanywa na mkandarasi kutoka kampuni ya FESAM CONSTRUCTION LIMITED yenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam (mkandarasi mzawa).
Sambamba na hilo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Munisi, amesema kuwa kupatikana kwa fedha za mradi huo kunatokana na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Mhe. Anne Kilango la kuhakikisha Wananchi wake wanaondokana na changamoto ya upatikanaji wa Majisafi na salama.
Wananchi wa Kata ya Kihurio hawakuwa nyuma kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuanzisha Mradi huo kwani kukamilika kwake kutatoa suluhu ya adha wanayoipata kwa kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji kwenye mito.
“Tulikuwa na kilio cha muda mrefu cha kutafuta huduma ya Majisafi, Wamama walikuwa wakiamka alfajiri sana na kutembea umbali mrefu kutafuta huduma na kuacha kushughulikia uchumi. Ujio wa mradi huu umetupa matumain na tunaamini utatoa ustawi kwa maish yetu” alisema ndugu Pili Salim.
Utekelezaji wa mradi wa Maji Kihurio unahusisha ujenzi wa miundombinu mipya kama vile ulazaji mabomba yenye urefu wa kilomita 54.9,ujenzi wa tenki kubwa lenye ujazo wa lita laki tano na ujenzi wa vituo 51 vya kuchota maji pamoja na kukarabati matenki yaliopo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...