-Yazindua Mauzo ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia kuboresha barabara Vijijini, mijini


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa madhubuti wa Rais DK.Samia Suluhu Hassan Masoko ya Mitaji Tanzania yamekuwa imara, himilivu na yenye mafanikio makubwa, licha ya uwepo wa athari za janga la UVIKO-19 na migogoro ya kiuchumi ya kimataifa.

Pia thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 47.5 na kufikia Sh. trilioni 45.86 katika kipindi kilichoishia Oktoba mwaka 2024, ikilinganishwa na Sh.trilioni 31.10 katika kipindi kilichoishia Oktoba 2021 wakati mauzo ya hisa na hatifungani katika Soko la Hisa yameongezeka kwa asilimia 51.48 na kufikia Sh. trilioni 9.93, ikilinganishwa na Sh.trilioni 6.55.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mauzo ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara Vijijini na mijini nchini ,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama amesema pia thamani ya nifuko ya uwekezaji wa pamoja imeongezeka kwa asilimia 253.7 na kufikia Sh. trilioni 2.48, ikilinganishwa na Sh. bilioni 701.46; na ndani ya kipindi cha miezi sita.

Ameongeza CMSA imeidhinisha Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kumi (10) inayotoa fursa ya uwekezaji kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, vikundi vya kijamii na mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Tunakushukuru na kumpongeza Rais kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa na matokeo chanya katika kukuza Thamani ya uwekezaji; na Thamani ya mauzo katika Masoko ya Mitaji."

Akielezea zaidi amesema katika uongozi wa Rais Dk. Samia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Chini ya Miongozo na malezi mazuri ya Wizara ya Fedha, yanayotolewa na Waziri wa Fedha, DK. Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu Dk. Natu Mwamba, imetekeleza mikakati ambayo imewezesha utoaji wa bidhaa mpya na bunifu zinazowezesha Kampuni na Taasisi kupata fedha za kuendeleza na kukuza biashara; na kugharamia shughuli za maendeleo.

Amesema utoaji wa bidhaa hizo umewezesha masoko ya mitaji Tanzania kuweka ALAMA SITA za Kwanza za kihistoria za mafanikio Kusini mwa Jangwa la Sahara yaani Sub Saharan Africa; na kuwezesha masoko ya mitaji Tanzania kuwa katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa mpya na bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani na kimataifa.

Ametaja baadhi ya bidhaa hizo ni hatifungani ya kwanza ya kijani yenye thamani kubwa na iliyotolewa katika fedha mbalimbali, Kusini mwa Jangwa la Sahara,Hatifungani ya kwanza yenye mguso na matokeo chanya kwa Jamii iliyotolewa katika fedha mbalimbali Afrika;

Nyingine ni Hatifungani ya kwanza yenye mguso wa jinsia Kusini mwa Jangwa la Sahara, Hatifungani ya kwanza inayokidhi misingi ya Shariah, Hatifungani ya kwanza ya kijani ya taasisi ya umma kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira na hatifungani ya kwanza iliyotolewa na shule ya sekondari ya wasichana na ambayo inakidhi misingi ya Shariah.

CPA Mkama amesema Mamlaka hiyo inampongeza Rais Samia kwa kuweka mazingira wezeshi yenye maono ya mageuzi na mabadiliko ambayo yameleta mafanikio hayo makubwa ya kuiweka Tanzania kwenye ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa bunifu zinazovutia wawekezaji wa ndani na kimataifa.

Kuhusu Uzinduzi wa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia yaani Samia iliyozonduliwa leo , amesema inaifanya Tanzania kuwa na ALAMA SABA za kwanza za kihistoria za mafanikio Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kuwa na hatifungani ya kwanza yenye ubunifu unaojumuisha vipengele vinavyogusa taasisi za umma na taasisi binafsi, ujenzi wa miundombinu ya barabara ngazi ya wilaya vijijini na mijini, inayotekelezwa na kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania zenye uwezo wa kujiendesha kibiashara.

Aidha amesema hatifungani hiyo inaweka msingi madhubuti wa kuonyesha njia kwa taasisi katika sekta ya umma na binafsi namna ya kupata fedha za kugharamia miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara, kupitia masoko ya mitaji.

"Mafanikio haya yametokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wako madhubuti Mheshimiwa Rais.Pia sera za uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wako Rais DK.Samia zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa zaidi katika masoko ya mitaji.

Pamoja na hayo amesema wanaipongeza Serikali kwa kuwezesha masoko ya mitaji Tanzania kufikia mafanikio hayo ya kihistoria huku akitoa taarifa kuwa CMSA imeidhinisha Waraka wa Matarajio wa Benki ya CRDB kuuza Hatifungani ya Miundombinu ya Samia yaani Samia yenye thamani ya Sh.bilioni 150.

" Idhini imetolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani. Mhe. Rais, napenda kutumia fursa hii kuufahamisha umma kuwa, Hatifungani hii imekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji.

"Lengo kuu la Hatifungani hii ni kuwawezesha wakandarasi wa ndani ambao wanafanya kazi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa na uwezo wa kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na wakati miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini hapa nchini,"amesema CPA Mkama.

Pia amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

Aidha amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi uliozinduliwa rasmi na Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba na unasimamiwa na Dk.Natu Mwamba ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Amefafanua hatifungani hiyo pia inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zitakazopatikana zitatumika kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi; na wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo kuinua vipato vyao.

"Tunakupongeza kwa kuwekwa mazingira bora, endelevu na yenye tija kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuinua vipato vyao; na kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi.

"Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Bodi na Uongozi wa Benki ya CRDB na Bodi na Uongozi wa TARURA na wataalam katika masoko ya mitaji waliowezesha kukidhi matakwa ya Sheria, taratibu na Kanuni za Uuzaji Hatifungani kwa umma. Ninatambua kwamba, kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini tumeweza kufanya kazi vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa,"amesema CPA Mkama.

Ametumia nafasi kusisitiza kwa ujumla, Masoko ya Mitaji nchini ni imara, himilivu na yenye mafanikio makubwa, kama ilivyodhihirishwa na ongezeko la thamani ya uwekezaji na mauzo katika soko la hisa na uwepo wa bidhaa mpya na bunifu. Mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...