Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha 22/11/2024
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Kitte Mfilinge, amesema kuwa heshima ya kila Mtanzania na mwanaCCM ni kuimarisha umoja kwa lengo la kufanikisha ushindi wa kishindo kwa kuchagua wagombea wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Mfilinge alibainisha kuwa CCM imejibu changamoto nyingi za wananchi kwa kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi kampeni za CCM kwa ajili ya uchaguzi huo kwenye viwanja vya Kwambonde, Mjini Kibaha, Mfilinge alisema wagombea wa CCM wameandaliwa vema na wana uwezo na ni bora kwenye uongozi .
Alisisitiza kuwa ni muhimu kuandaa timu bora kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa ili kushirikiana na madiwani, wabunge, na viongozi wengine katika kuimarisha maendeleo na uchumi.
“CCM ni chama chenye uzoefu mkubwa na uwezo wa kusimamia maendeleo. Ni chama pekee kilichowezesha mafanikio makubwa kwa wananchi,” alisema Kitte.
Aidha, aliwahimiza wagombea kufanya kampeni za kistaarabu kwa kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya CCM na mipango yao ya kuwahudumia wananchi.
Mfilinge pia alisisitiza umuhimu wa wananchi waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura na kufanya uamuzi sahihi kwa kuchagua CCM, akisema ni chama chenye ilani imara inayolenga kuwatumikia Watanzania kwa dhati.
Nae Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alieleza CCM imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati.
Alitaja mafanikio katika sekta ya afya, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 19 zimetumika Mjini Kibaha, zikiwemo ujenzi wa zahanati sita mpya, vituo vitatu vya afya, na maboresho ya hospitali ya wilaya kwa vifaa tiba.
Katika sekta ya elimu, Koka alibainisha kuwa shule mpya saba zimejengwa, ikiwemo shule za sekondari nne na za msingi tatu, kupitia fedha za Serikali.
Pia alizungumzia sekta ya miundombinu, akisema kuna mpango wa kujenga barabara za lami katika kila kata, mpango ambao tayari umewasilishwa TANROADS na TARURA na upande wa Nishati ya umeme Vijijini unaendelea kuenezwa kila kona.
“Hatutegemei kushindwa kwa sababu utekelezaji wa Ilani yetu umekuwa na matokeo chanya kwa wananchi wa Kibaha na miji mingine nchini,” alisema Koka.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwl. Mwajuma Nyamka, alifafanua ,CCM Kibaha Mjini iko tayari kwa uchaguzi na inalenga kushinda mitaa yote 73 ambapo hadi sasa, kati ya mitaa hiyo, 35 itapigiwa kura ya “Ndiyo” au “Hapana” kutokana na kukosa upinzani, huku mitaa 38 ikiwa na ushindani.
“Tumejipanga kwa ushindi wa heshima kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanikisha utekelezaji wa Ilani kwa zaidi ya asilimia 95 mjini hapa,” alisema Nyamka.
Kampeni za vyama vya siasa zinaendelea kwa mujibu wa sheria na taratibu kuelekea uchaguzi wa Novemba 27, 2024, ambapo kila Mtanzania aliyejiandikisha anahimizwa kushiriki kupiga kura kwa ajili ya kuleta maendeleo chanya katika mitaa, vijiji, na vitongoji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...