Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya Zanzibar na Jamhuri ya watu wa China kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili .
Ameyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Gavana wa Jimbo la ZHEJIANG Bwana. YANG QINGJIU na ujumbe wake waliofika ofisini kwake Vuga kumtembelea.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China katika kuisaidia Zanzibar kupitia nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya Afya, Kilimo, Elimu na Habari pamoja na miradi mbali mbali ya kimkakati jambo lililopelekea kuimarika kwa huduma katika sekta hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya watu wa china kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar kupitia Nyanja mbali mbali ikiwemo kupokea madaktari Bingwa kutoka nchini China ambao husaidia kutoa huduma za tiba na ushauri kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali mbali mbali ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha, Mhe. Hemed amemueleza kuwa kipaombele cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Uchumi wa Buluu ambao unajumuisha mambo mbali mbali ikiwemo Sekta ya Utalii ambayo imekuwa ikiichangia pato kubwa la Serikali kutokana na ongezeko la wageni wengi wanaoitembelea Zanzibar.
Sambamba na hayo, Mhe.Hemed ameikaribisha Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China kupitia uongozi huo wa Jimbo la ZHEJIANG kuja kuekeza Zanzibar na kuzitumia fursa mbali mbali zilizopo nchini ikiwemo uchumi wa buluu.
Nae Naibu Gavana kutoka Jimbo la ZHEJIANG nchini China Bwana. YANG QINGJIU amesema wameamua kuja Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili hasa katika masuala ya maendeleo.
Bwana. YANG QINGJIU amesema China imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya uchumi, Utamaduni na elimu kwa kuwapatia wazanzibari ufadhili wa masomo ya muda mrefu na mafunzo ya muda mfupi hasa katika kada mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwaongezea maarifa watumishi wa umma.
Amesema Jimbo la ZHEJIANG limepiga hatua kubwa sana katika masuala ya biashara hivyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanawawekea mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...