Na  Mwandishi Wetu, Michuzi TV


NAIBU  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma amesema kuwa ili kufikia azma ya kuwa kitovu cha madini barani Afrika ni lazima kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa za mwisho tayari kwa soko la ndani na nje ikiwemo masoko makubwa duniani. 

Amesema kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2024 uliofanyika kwa siku tatu ambapo ameeleza pia kupitia mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu masuala mengi yanayohusu sekta ya madini yamejadiliwa.

"Mijadala  iliyofanyika kupitia mkutano huu imejikita kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya madini, hususan katika nyanja za mitaji na teknolojia ya kisasa katika uongezaji thamani madini ...

"Na kupitia maazimio yaliyotolewa na washiriki, Serikali imepata mapendekezo yatakayofanyiwa kazi kwa manufaa ya sekta  na taifa kwa ujumla,"amesema Naibu Spika Mgeni aliyekuwa amemwakilisha Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Ameongeza kwamba uongezaji thamani madini ni jambo la msingi kwa maendeleo yetu,hivyo inapaswa  kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa za mwisho tayari kwa soko la ndani na nje.

Pia amesema katika mkutano huo Kampuni mbalimbali zinazoshughulika na mnyororo wa thamani wa madini zimepata nafasi ya kushiriki mkutano huo, na kwamba matumaini yake ni kuwa zimejifunza kwa kina kuhusu Sera za Madini za Tanzania hivyo zitaendelea kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya sekta ya madini hapa nchini. 

Wakati huo huo Naibu Spika Mgeni ameipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa juhudi zake za kufanya utafiti wa madini visiwani Zanzibar na kisha kuandaa ramani ya jiolojia ya visiwa hivyo.

Amesema kuwa kupitia ripoti ya utafiti wa madini visiwani Zanzibar iliyokabidhiwa na GST hivi karibuni visiwani humo, imesaidia kujua utajiri mkubwa wa rasilimali madini uliopo Zanzibar iko tayari kuendeleza rasilimali madini yaliyoanishwa kwa mujibu wa Sheria. 

Awali Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesisitiza kuwa, Mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa, kwani kwa mwaka 2024 umeleta washiriki zaidi ya 1500 kutoka Afrika na nje ya Africa kwa nia ya kubadilishana uzoefu.

“Kutokana na mahudhurio makubwa ya washiriki, tunafikiria kuwa na eneo letu maalum kwa ajili ya Mikutano ya Sekta ya Madini kama ilivyo kwa Mining Indaba kule Afrika Kusini, na ninawaomba Wakuu wa Mikoa kutenga maeneo maalum katika mikoa yao kwa ajili ya mikutano hii ya madini” amesema.

Kuhusu Sekta ya Madini visiwani Zanzibar,  Mhe. Mavunde amesema “Watu wakisikia Zanzibar wanachofikiria ni utalii, lakini miezi michache iliyopita Ripoti ya Utafiti wa Madini kule Zanzibar, Pemba yamegundulika madini tembo (Heavy Mineral Sands) hivyo kupitia rasilimali hiyo tunaamini uwekezaji mkubwa utafika pemba na tutaona manufaa ya uwepo wa rasilimali hizo na itasaidia kufungua uchumi wa Zanzibar“

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Nishati na Madini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shaib Hassan Kaduara amesema kama taifa moja ni muhimu kuimarisha ushirikiano katika eneo la utafiti wa kina wa madini kwa manufaa ya pande zote na kuongeza kuwa “Ni fahari kubwa kujua tuna rasilimali hizi na tunaahidi kuzisimamia kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo”

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kaulimbiu ya mkutano ilikuwa inasema  “Uongezaji Madini Thamani kwa Maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii  ikiwa na lengo la kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini kwa maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii.

Amebainisha kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Madini ya 2009 inayoitaka  Serikali kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi ili kupanua wigo wa mnyororo wa thamani kupitia fursa za ajira na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini nchini.

Katika mkutano huo wa Kimataifa ambao umehusisha nchi mbalimbali umeelezwa  kuwa na mafanikio makubwa na idadi ya walioshiriki ni zaidi ya wadau 1500 katika sekta ya madini na idadi hiyo ya washiriki ni kubwa ukilinganisha na mikutano iliyopita.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...