Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini kwa lengo la kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo kwani kuna fursa nyingi katika madini huku ikiweka wazi mkakati wa kuendelea kuwainua wachimbaji wadogo ili nao wakue na kuwa wachimbaji wa kati ifikapo mwaka 2030.

Pia amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuongeza mchango wake na hasa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuhakikisha sekta hii inachangia asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 sambamba na kuweka mkakati wa kuhakikisha shughuli za uongezaji thamani ya madini zinafanyika nchini ili kuongeza tija ya ukuaji wa maendeleo ya uchumi na kijamii.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Mkutano wa Kimataifa wa uwekezaji katika Sekta ya madini uliohusisha wadau kutoka mataifa mbalimbali akimwakilisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambapo ametumia mkutano huo pia kueleza kwa kina umuhimu wa sekta ya madini nchini na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira katika sekta hiyo.

"Ndugu washiriki wa mkutano huu wenye kauli mbiu inayosema Uongezaji Thamani ya Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii, tunawahakikishia lengo la Serikali ya Tanzania ni kuendelea inachukua hatua mbalimbali katika kuongeza thamani ya madini na kauli mbiu ya mkutano huu imelenga kuhamasisha katika shughuli zote za madini kuwa na thamani.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana barani Afrika zenye uzalishaji mkubwa wa madini hususani dhahabu lakini bado nchi yetu hainufaiki kwasababu shughuli nyingi za uongezaji thamani katika madini zinafanyika nje ya nchi yetu.

"Ni dhahiri kwamba Taifa linakosa mapato katika mnyororo wa thamani na hivyo kwa kutambua manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi katika uongezaji thamani madini Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo upitiaji sera,sheria, kanuni pamoja na miongozo mbalimbali ambayo itakwenda kushughulikia hasa katika eneo la uongezaji wa thamani ya madini ambapo sasa tunataka kuona shughuli hizo zinafanyika hapa hapa nchini ."

Waziri Mkuu amesisitiza lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuongeza mchango wake na hasa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuhakikisha sekta hiyo inachangia asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 .Mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umekuwa na kukua huku ni kutokana na ongezeko la asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.

"Ni matumaini yangu ifikapo mwaka 2025 sekta ya madini itafikia lengo la mchango wa asilimia 10 katika pato la ndani la Taifa.Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii Serikali imechukua hatua ya kuhamasisha wawekezaji wakubwa na wadogo katika sekta ya madini wanaendesha shughuli zao kwa tija na kuwezesha mazingira wezeshi ikiwemo uwekezaji na upatikanaji wa teknolojia unaimarika na hii ni pamoja na kuimairisha miundombinu mbalimbali ili kuvutia uwekezaji na kuwezesha uwekezaji huo kuleta faida kwa kila mwekezaji.

"Hatua ambazo tumechukua ni kuongeza uwezo wa nishati ya umeme katika gridi ya Taifa, pia kuimarisha njia za usafiririshaji kama vile barabara ,reli,bandari na kuongeza ndege na kujenga Viwanja zaidi,yote haya ni katika kusaidia shughuli za uendeshaji katika sekta ya madini.Tunapoendelea kuimarisha hayo pia tunaendelea kuimarisha Masoko.Serikali imeshafanya kazi kubwa katika eneo hili ,imesogeza huduma na sasa tuna Masoko 44 nchini na vituo 143 vya kununulia madini hapa nchini."

Kuhusu kutano huo wa sita wa Kimataifa katika Uwekezaji katika sekta ya madini amesema wadau kutoka watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuonesha teknolojia zinazotimika katika uchimbaji madini.

Amesisitiza lengo mahususi la mkutano huo ni kuvutia uwekezaji kutoka nje kuja nchini Tanzania na limekuwa jukwaa la kuvutia wawekezaji wengine zaidi kutoka nchi rafiki kote duniani ambako kuna rasimali na teknolojia za kisasa vitakavyowezesha sekta ya madini hapa nchini

"Tunaamini kupitia mkutano huu tutabadilishana mawazo, uzoefu na teknolojia bora katika sekta ya madini ,hatua hii ni muhimu sana katika kuboresha utendaji katika sekta ya madini lakini pia kuhimiza matumizi Bora ya rasilimali zilizopo lakini dhumuni lingine ni kukuza usimamizi bora wa rasilimali za madini zilizopo."

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini yamechochewa na uongozi bora wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na amebainisha kuwa serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka Shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231 ili kuimarisha zaidi sekta hiyo.

Amefafanua kuwa Rais Dkt. Samia ametoa maelekezo ya mashine mbili za uchorongaji kupelekwa kwa wanawake wachimbaji ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi huku akiweka wazi mkakati uliopo ni kununua mashine za uchorongaji 15 ambazo zitapelekwa katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji kuwawezesha wachimbaji nchini.

Akielezea kuhusu sera mpya ya kuongeza thamani ya madini inalenga kutoa ajira kwa vijana wengi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa huku akisisitiza mkutano huo utatoa nafasi ya wadau kujadiliana masuala yanayohusu sekta ya madini na ametumia nafasi hiyo kueleza wachimbaji wadogo huu wa kimataifa umeleta fursa ya kuimarisha watapata maeneo ya uchimbaji baada ya Serikali kufuta leseni 2000.

Awali Victor Tesha ambaye ni Makamu Wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania amesema wanaipongeza Serikali chini ya Rais DK Samia Suluhu Hassan kwa hatua wanachukua kuboresha sekta ya madini na kubwa zaidi wanashukuru kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakipewa nafasi ya kusikilizwa wanapowasilisha changamoto zao kwa Serikali.

"Sifa kubwa ambayo mwanadamu anaitaka ni kumsikiliza na ukweli Serikali imekuwa ikitukimbilia.Tunaomba leseni za wachimbaji wadogo kwani tunafahamu Serikali imefuta leseni 2000 hivyo tunaomba leseni hizo kwa wachimbaji wadogo.Kwa sasa wachimbaji wadogo tunachangia asilimia 40 ya pato la taifa na lengo letu ni kufikia asilimia 60."











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...