Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewahimiza Mawakili wapya wa kujitegemea walioapishwa leo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, maadili, na miiko ya taaluma yao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Mawakili hao iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Johari aliwataka wazingatie umuhimu wa kujiendeleza kielimu na kitaaluma ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia na kuchangia kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
“Nawaomba mfanye kazi zenu kwa kuzingatia weledi, maadili, na taratibu zinazowaongoza. Ni muhimu pia mkaendelea kusoma na kujifunza ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kitaifa na kimataifa,” alisema Johari.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, jumla ya Mawakili 524 wa Kujitegemea waliapishwa rasmi. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza nguvu kazi ya wanasheria nchini, huku ikitarajiwa kuwa watachangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa haki na kuimarisha mifumo ya kisheria nchini.
Hafla hiyo pia ilitumika kuwakumbusha Mawakili hao juu ya jukumu lao la kuilinda taaluma ya sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote bila upendeleo. Profesa Juma alisisitiza kuwa kazi ya uwakili siyo tu huduma bali pia ni wito wa kuhudumia jamii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...