Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amekutana na kufanya mazungumzo na Prof. Gerald Eisenkopf, wa Chuo Kikuu cha Vechta nchini Ujerumani ambacho kimekuwa na ushirikiano na UDOM toka mwaka 2023, kupitia Idara Sosholojia na Anthropolojia iliyopo Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii (CHSS).
Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Jengo la Benjamin Mkapa, Dodoma, leo tarehe 30 Januari 2025. Katika Mazumgumzo hayo Prof. Kusiluka ameeleza malengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma ya kuongeza wigo wa ushirikiano na Chuo hicho na hasa kwenye maeneo yanayohusu Uchumi wa Afya kwa kuanzisha programu za Shahada za Uzamili kwa ushirikiano na Chuo hicho.
“Katika kuhakikisha Chuo chetu kinatekeleza kwa vitendo Ukimataifaji, tumejizatiti kuhakikisha tunaanzisha shahada za pamoja na washirika wetu, usimamizi wa pamoja wa Tasnifu, pamoja na kuanzisha programu za masafa “ on line” ili watanzania wengi waweze kunufaika na Chuo chao kwa kupata mafunzo popote walipo” alisisitiza
Aidha amewataka wataalamu wanapofanya mapitio ya Mkataba wa Makubalino na Chuo Kikuu cha Vechta, kupanua wigo kwa kuhakikisha Idara zingine zilizopo ndani ya Chuo hicho zinanufaika na ushirikiano huo.
Kwa upande wake Prof. Gerald Eisenkopf, ameshukuru kwa utayari wa UDOM kushirikiana na Chuo cha Vechta, na kwamba suala la ufudishaji kwa njia ya mtandao kwa sasa haliepukiki na Chuo chake kiko tayari kuendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma. Aidha, amesema wako tayari kuanzisha pogramu za pamoja kwa kutumia wataalamu walionao, kuendelea kubadilishana wataalamu, kuanzisha usimamizi wa pamoja wa Tasnifu pamoja na kufanya utafiti na kwamba daima watakuwa tayari kutoa msaada kadiri utakavyohitajika.
Kupitia ushirikiano huo tayari mfanyakazi mmoja amepata udhamini wa masomo ya Shahada ya Uzamivu kupitia mpango wa mafunzo. Maeneo mengine yaliyoazimiwa kuboreshwa ni kuandika miradi ya pamoja ya utafiti pamoja na Kujenga uwezo wa tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa Shahada za Uzamivu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Razack Lokina, RASI wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, Prof. Albinus Tenge, RASI wa Ndani ya Biashara na Uchumi Prof. Ismail Ismail, Dkt. David Mrisho wa Chuo Kikuu cha SAUT ambao nao wana ushirikiano na Chuo hicho, pamoja na wakuu wa Idara ambazo Chuo Kikuu cha Vechta, kinatekeleza makubaliano ya ushirikiano.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, akizungumza na Prof. Gerald Eisenkopf, wa Chuo Kikuu cha Vechta nchini Ujerumani, alipotembelea ofisini kwake.

Prof. Gerald Eisenkopf akizungumza wakati alipokutana na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Kusiluka. Pembeni ya Gerald ni Prof. Ismail Ismail, Mkuu wa Ndaki ya Biashara na Uchumi.

Prof.Kusiluka akimkabidhi zawadi ya ukumbusho Prof. Gerald Eisenkopf

Hapa wakibadilishana mawasiliano na kuagana, baada ya kumaliza mazungumzo. Kushoto ni Prof. Razack Lokina ( Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma) na katikakati ni Prof. Albinus Tenge ( Mkuu wa Ndaki ya Insia).

Prof. Kusiluka(katikati), Dkt. David Mrisho wa Chuo Kikuu cha SAUT (kulia), Prof. Gerald Eisenkopf (kushoto), wakiwa akiwa na ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika picha ya pamoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...