MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu imemuhukumu mfanyabiashara, Khamis Luwongo (45) kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya aliyekuwa mke wake Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Awali,Luwongo alijaribu kuizuia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutomsomea adhabu yake hadi atakapozungumza yeye hali hiyo ilisababisha taflani kati ya mshtakiwa na Jaji Hamidu Mwanga, baada ya mshtakiwa kutaka kutumia mabavu kuzungumza anachokitaka yeye baada ya wakili wake kumaliza kuiomba Mahakama ipunguzie adhabu mteja wake.

Hukumu hiyo imetolewa Leo Februari 26,2025 na Jaji, Hamidu Mwanga na kabla ya kutoa adhabu hiyo alitoa maelezo yaliyopelekea mshitakiwa kukutwa na hatia katika kosa hilo.
 Jaji Mwanga alisema mshitakiwa alitia hatiani kwa kosa hilo kutokana na ushahidi uliotolewa na mashihidi 14 pamoja na viellezo kikiwemo melezo ya onyo ambayo mshitakiwa alichukuliwa akiwa katika kituo cha polisi.

Jaji Mwanga amesema kuwa katika ushahidi uliotolewa ilidaiwa kuwa kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Hamisi na mkewe Naomi na baadae marehemu alidaiwa kupotea, katika kupotea huko Hamisi alitoa taarifa za kutoonekana kwa mke wake ikiwemo katika vituo vya polisi.

Akiwa anaendelea kufuatilia taarifa za mke wake Hamisi alidai kuwa alitumiwa ujumbe kutoka kwa Naomi akimwambia kuwa aliamua kwenda nje ya nchi hivyo alimtaka awe analea mtoto wao.

Ilidaiwa kuwa Julai 16,2019 katika kituo cha polisi cha kati wakati Hamisi akiwa anaendelea na harakati za kutoa taarifa polisi juu ya maendeleo ya mke wake alihojiwa kuhusu jumbe alizodaiwa kutumiwa na mke wake kwani kwa uchunguzi wa kielektroniki ilionyedha kuwa jumbe hizo zilitumwa katika sehemu moja.

Aidh, Jaji amesema ni jukumu la upande wa mashitaka kuthibitisha hatia ya mshitakiwa na katika mauaji inatakiwa kuthibitishwa kama mtu kweli amekufa na kifo chake kuwa sio cha kawaida.

Amesema katika kesi kuna mazingira tofauti kidogo na mazingira yake yanaonyesha kuwa hakukuwa na mwili kuthibitisha kuwa kweli Naomi amekufa na kama hakuna mwili basi uchunguzi wa kitabibu haukufanyika kubaini marehemu alikufa kwa sabbau au kutokana na nini.

Ameongeza kuwa kutokana na kesi zilizothibitishwa kutoka nchini India zilionyedha kuwa kifo cha mtu kinaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira ambayo kifo hicho kimetokea na uchunguzi unaweza kufanyanyika pasipokuwa na mwili.

“Sio lazima kuwe na mwili ikiwa ni suala la lazima kuwepo na mwili ili kuthibitisha hatia tutawapa watu upenyo wa kuteketeza ili kukimbia ushahidi,” amesema Jaji Mwanga.

Pia amesema kuwa katika mashahidi hao wapo waliokwenda Morogoro na kwa upande wa mkemia alileta majibu kuwa alishindwa majibu ya moja kwa moja kwani ilibainika mabaki yaliyopatikana yalikuwa ni ya mwanamke lakini haikuthibitihshwa kuwa ni ya Naomi .

Jaji Mwanga amesema kuwa katika maelezo ya onyo ya Hamisi alidai kuwa mabaki yale ni ya ya Naomi na alidaiwa kuwa Naomi amefariki na mshitakiwa ndiyo aliyemuua na pia chumba alichokuwa akilala Naomi kilikutwa na mabaki ya damu na yalidaiwa kuwa ni ya Naomi.

Pia kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya mshitakiwa alidai kuwa Mei 14,2019 ni siku ambayo hakulala nyumbani kwake kwani alilala kwa Margreth alirudi kwake asubuhi na kumkuta mke wake akimuandaa mtoto kwenda shule alidai alimpita bila kusema chochote na mtoto alichukuliwa na bodaboda kupelekwa shule.

Aliendelea kudai kuwa simu iliita kwa jina la Magreth ndipo Naomi alianza kumtukana na Hamisi akamwambia achukue chochote anachokitaka kwani hakukuwa na ndoa tena kati yao wakati wa ugomvi Naomi alidondoka chini na kujigonga kichwani na damu zikaanza kutoka akawa analalamika akitetemeka sitomsamehe.

Baadaye alianza kukoroma hadi umauti ulipomfika baada ya Naomi kufa Hamisi akataka kuundoa mwili ndipo alipouzungusha kwenye shuka mbili na baada ya kuona kuwa akitoka na mwili ule kwenye gari akiwa barabarani askari wangemsimamisha na kuuona ndipo alipokumbuka katika banda la kuku kulikuwa na shimo kwa ajili ya kupitisha maji.

Alipokumbuka hili alichukua mwili na kwenda kuuchoma na magunia mawili ya mkaa ili uungue taratibu kwani alihofia kuchoma na kuni zingekuwa nyingi na wakati mwili ulipoungua na kubaki mkaa alimtuma bodaboda kwenda kununua mafuta na alipofiki alikwenda kuyachukulia getini ili asiingie ndani.

Pia jaji aliendelea kusema kuwa maelezo hayo yanaeleza kuwa kwakuwa mafuta ya taa yangeisha haraka akachukua viatu na kuviweka ili uendelee kuungua taratibu na baada ya hapo alichukua mabaki na majivu na kupanda gari yake aina ya Subaru na kuondoka hadi shambani kwake Morogoro ndipo alipofukia na kupanda Mgomba juu ya mabaki hayo.

Jaji amesema hakuna mtu anayeweza kutoa mtiririko huo wa matukio isipokuwa tu yule anayejua ukweli wa tukio hilolilivyotokea, hivyo alisema kuwa maelezo hayo ni ya kweli na ya kuaminika.

Pia amesema kuwa ushahidi uliotolewa na shahidi namba nne ambaye alikuwa ni Mpwa wake ni wa kuaminika kwani hakuwa na sababu ya kumuongelea uongo mjomba wake kwa sababu ndiye aliyemtoa kijijini kumleta Dar es salaam kwa ajili ya kufanya kazi.

"Kwenye maelezo haya ya onyo mshtakiwa anaeleza vizuri sana hadi alivyochukua laini za mke wake akaanza kujitumia ujumbe mfupi na pia amesema alitoa taarifa kwa ndugu wa marehemu kuwa Naomi amesafiri nje ya nchi," amesema Jaji Mwanga


Baada ya mshitakiwa kukutwana hatia alipata nafasi ya kujitetea na katika utetezi wake alidai kuwa maelezo hayo ya onyo yalikuwa si ya kwake na jaji alisema mahakama ilitupilia mbali kwani hakukataa maelezo hayo mara ya kwanza yalipoletwa kama kilelezo mahakamani.

Amesema pia mahakama inaangalia baada ya mauaji ni kitu gani kilitendeka na kwa mujibu wa maelezo maada ya mauaji aliviringisha mwili kwenye shuka mbili na kwenda kuuchoma na kwa mujibu wa maelezo hayo inaonyesha mshitakiwa alidhamiria kutenda kosa.

Pia mawakili wa mshitakiwa walidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa akiwa hana akili timamu na alichukuliwa na kupimwa uwezo wake wa kufikiri lakini kutokana na mtiririrko ulivyojieleza mshitakiwa alionekana kuwa na akili timamu kwani aliweza kufikiria kutenda matukio yote.

Jaji alisema kuwa mahakama hiyo ilimtia hatiani mshitakiwa kwa kumuua mke wake chini ya kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya adhabu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mzava alieleza mahakama kuwa mshitakiwa hana rekodi ya makosa ya nyuma lakini aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe funzo kwa wanaume wote kwani kifo cha Naomi kimeonyesha kuambatana na mateso makali na kufanya vijana na watu wengine kuwa na hofu kuingia katika ndoa.

"Kuna jambo kubwa la kujifunza hapa kifo chake kilikuwa cha kikatili , mateso, alikufa kifo cha kinyama hata jamii inajiuliza anawezaje kufanya tukio kama hili,"alidai Mnzava akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu Yasinta Peter

Pia aliiomba mahakama ikabidhi kielelezo namba PW8 ambacho ni mabaki wa mwili wa Naomi kwa familia yake ili aweze kupewa heshima ya mwisho ya kidini ambayo hakupewa baada ya kifo chake.

Jaji Mwanga alisema hilo ni kosa la mauaji mikono yake imefungwa kiapo chake cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sheria za Tanzania adhabu ni moja tu kunyongwa hadi kufa.

"Nina muhukumu Khamis Luwonga maarufu kwa jina la Meshack adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake Naomi Marijani,"alisema Jaji Mwanga

Katika kesi hiyo ya mauaji namba nne ya mwaka 2019, Mshtakiwa Luwongo ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni alimuua Naomi Marijani.

Nje ya Mahakama

Baba mdogo wa Marehemu, Robert Marijani alisema wameridhika na hukumu ilitolewa maelezo aliyoyasema polisi ndiyo ndiyo hayo hayo

Mtoto wake alikuwa mpambanaji, mjasiliamali mchakalikaji, laknii mume wake (Meshack) alikuwa anataka awe tu mama wa nyumbani hakutaka ajishughulishe

Alisema walipomuwezesha mtoto wao kufanya biashara ndipo ikawa kero kwa mume wake kabla ya kifo hicho aliwahi kusuluhisha ugomvi baina yao lakini huwezi kujua akili ya mtu.

Aidha, wanatarajia kumzika Naomi upya, kwa kuchukua mabaki ya mwili ya mwili wake katika kesi hii hakuna mwili wa marehemu kwa sababu yeye alienda kuzika shambani wao wanachukua kwenda kumzika rasmi.

"Hatuwezi kumrudishia kwa sababu yeye aliamua kupandia migomba na wao wanataka kuzika rasmi,"alisema

Hata baadhi ya ndugu, walisema kwa sasa watapumzika kidogo kwa sababu walikuwa wakilia kila siku wakiiomba haki ipatikane ili wampumzishe Naomi katika nyumba yake ya milele kwa kuzika mabaki yake.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...