Nchi 28 zimekutana katika mkutano wa kimataifa wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) kwa ukanda wa Afrika, lengo likiwa ni kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti madawa na chanjo feki kwa mifugo.


Miongoni mwa mikakati iliyopendekezwa ni kuanzisha mifumo madhubuti ya usajili na ufuatiliaji wa dawa zinazoingizwa na kutumika, hatua ambayo itasaidia kuziondoa dawa na chanjo zisizo na viwango stahiki sokoni.


Akizungumza  wakati wa uzinduzi wa mkutano huo uliofanyika Machi 4, 2025  jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo) Bw. Abdul Mhinte amesema Tanzania iko tayari kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya dawa na chanjo feki za mifugo.


“Mkutano huu wa siku tatu, kuanzia Machi 4 hadi 6, utajadili mikakati mbalimbali ambayo wataalamu watachambua na kutoa maoni kuhusu namna bora ya utekelezaji katika kila nchi kulingana na taratibu zao,” alisema Mhinte.


Aidha Bw. Mhinte ameongeza kuwa mkutano huo ni muhimu kwa Afrika, kwani kumekuwa na ongezeko la dawa na chanjo feki, jambo lililosababisha WOAH kuandaa mkakati maalum wa kusaidia nchi za Afrika na dunia kwa ujumla kupambana na tatizo hili.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Dkt. Benezeth Lutege, alibainisha kuwa serikali imetenga Shilingi bilioni 28.1 kwa ajili ya kampeni ya kitaifa ya chanjo kwa mifugo, ambayo itazinduliwa hivi karibuni.


“Chanjo zitakazotumika mwaka huu ni zile zinazozalishwa ndani ya nchi na kukaguliwa na mamlaka za serikali, hatua ambayo itasaidia kuzuia uingizwaji wa chanjo na dawa feki zinazosababisha usugu wa magonjwa,” alisema Dkt. Lutege.


Aidha Dkt. Lutega aliwataka wafugaji, waingizaji wa dawa na chanjo, pamoja na wazalishaji, kuzingatia kanuni na taratibu za uzalishaji, usambazaji, na uuzaji wa dawa hizo.


Naye Jane Royelo kutoka WOAH aliwahimiza wafugaji na wauzaji wa dawa za mifugo kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhamasishwa matumizi sahihi ya dawa na kuepuka matumizi mabaya ya dawa zisizohitajika.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...