Songea-Ruvuma.

Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Songea ambaye ni Mstahiki Meya Mbano Michael, leo Aprili 30 ameongoza Baraza la Madiwani la robo ya tatu ya mwaka, na kuwataka Madiwani wa Manispaa hiyo kwenda kufanya vikao na tathmini katika Kata zao kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu ambayo bado ipo chini, licha ya Manispaa hiyo kufanya vizuri kwenye sekta nyingine.

Katika hotuba yake, Mstahiki Meya Mbano Michael alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio yanayoonekana katika sekta mbalimbali, hali ya elimu bado hairidhishi na inahitaji juhudi za ziada, amewataka Madiwani kwenda kwenye kata zao na kufanya tathmini ya hali halisi ya elimu, ikiwemo mahudhurio ya wanafunzi, na utendaji wa walimu, ili kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua, alisisitiza kuwa maendeleo ya Manispaa hayawezi kuwa endelevu bila msingi imara wa elimu bora kwa watoto ambao ndio viongozi wa baadae.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya TACTIC Meya Mbano alieleza kuwa miradi hiyo inaendelea kutekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Wizara ya TAMISEMI, Lengo kuu ni kuboresha miundombinu ya mijini ili kuongeza ushindani wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji. Alisema kwa sasa mkandarasi bado yupo kazini, na hakutakuwa na ongezeko la majukumu mapya hadi pale mradi wa awali utakapokamilika ipasavyo.

Kuhusu mikopo ya vikundi, amesema kuwa pamoja na kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali, changamoto kubwa imekuwa ni urejeshaji wa mikopo hiyo, ameeleza kuwa baadhi ya vikundi bado hawajarejesha mikopo waliyopatiwa, hali inayosababisha ugumu wa kutoa mikopo mingine, ambapo  Manispaa ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha mikopo ya awali inarejeshwa.

Aidha, ametoa shukrani kwa Madiwani, Wakuu wa Idara, Wananchi, Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na watumishi wote waliomsaidia katika kutekeleza majukumu tangu mwaka 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, ameeleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa soko la Manzese umefikia asilimia 95 na asilimia 5 pekee ndiyo imebaki kukamilisha mchakato huo kabla ya kusaini mkataba na kuanza kwa ujenzi mwezi wa tano.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Amandus S. Chilumba alisema Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefikia takribani asilimia 90 ya makusanyo ya mapato, ameeleza kuwa hadi kufikia Aprili 17, zaidi ya shilingi milioni 384 zilitumika kama marejesho ya fedha katika shughuli mbalimbali.

Amesema zaidi ya milioni 129 bado ni marejesho yaliyoko ndani ya muda, huku zaidi ya milioni 254 yakiwa ni marejesho yaliyopitiliza muda wa kurejesha, ametoa wito kwa wakuu wa idara wakiongozwa na Mkurugenzi kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili kuepusha changamoto.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Songea, James Mgego, aliwapongeza Madiwani kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitano, Alisema CCM inataka mabadiliko na amefurahishwa na mazingira rafiki ya utendaji kazi, ametoa rai kwa Madiwani kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili waweze kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan kwa kishindo.






 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...