Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ipo mbioni kuanza ujenzi wa reli ya Jiji la Dar es Salaam (Commuter Rail Network) ndani ya miaka 30 ijayo.

Kadogosa amebainisha hayo wakati akitoa wasilisho katika kikao kazi cha pamoja baina ya Menejimenti ya TRC na Wanahabari wa mitandao ya jamii, kinachofanyika mkoani Morogoro ambapo kinalenga kutoa elimu, maarifa na stadi za namna bora ya kuripoti habari za Reli.

CRN ni mtandao wa reli unaohusisha usafiri wa treni zinazotumika kubeba abiria kwa umbali mfupi hadi wa kati, hasa katikati ya miji na maeneo yake ya pembezoni.

Utekelezaji wa mradi huo,utahusisha treni zinazofanya safari kwa njia za umma ambapo abiria watakuwa wakitumia treni kusafiri kwenda na kurudi kutoka kazini, biashara, vituo vya afya, shuleni, nyumba za ibada na kwingineko.

Kadogosa amesema, utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji huduma bora za usafirishaji kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo ya jamii na Taifa.

"Kwa hiyo, reli ya Dar es Salaam ni must,"amesema Kadogosa huku akibainisha kuwa, uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na Taifa.

Amesema, utekelezaji wa treni za namna hiyo utaenda jijini Dodoma na huko utaanza mapema zaidi, na baadaye utaelekea Arusha na Mbeya.

"Usanifu wa awali na upembuzi yakinifu umekamilika kwa upande wa ujenzi wa Reli ya Jiji la Dar es Salaam, pia Dodoma umekamilika, na tutaanza mapema zaidi, kwa sasa hatua za utafutaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli zinaendelea."

Kadogosa amesema, miradi hiyo inatarajiwa kufanyika kwa kushirikisha sekta binafsi (PPP) ambapo kampuni mbalimbali zimejitokeza. "Na zimeonesha nia ya kushiriki katika ujenzi wa njia hizo ikiwemo Kampuni ya Alstom."






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...