Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaendelea na juhudi za kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji nchini kote. Katika jitihada hizo, TEA imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la Bodi ya Maktaba lililopo kisiwani Pemba. 

Ukarabati huu unalenga kuimarisha miundombinu ya taasisi hiyo muhimu inayotoa huduma kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza katika ziara ya ukaguzi kisiwani Pemba, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA, Bw. Masozi Nyirenda, alieleza kuwa fedha hizo tayari zimetolewa. 

Alibainisha kuwa ukarabati utaanza mara tu baada ya mkandarasi kusaini mkataba rasmi na kuwasilisha mpango kazi utakaoonesha hatua kwa hatua namna kazi hiyo itakavyotekelezwa hadi kukamilika kwa wakati.

Mradi huu wa ukarabati unatekelezwa kama sehemu ya majukumu ya TEA kama taasisi ya Muungano, ambayo kimsingi inahusika na utafutaji wa rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu. 

Kupitia miradi kama hii, TEA inalenga kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia bila kujali eneo analotoka.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Bodi ya Maktaba Pemba, Bw. Ahmed Hamis, jengo linalotarajiwa kukarabatiwa ni miongoni mwa majengo ya kihistoria yaliyojengwa kipindi cha ukoloni. 

Hata hivyo, tangu lijengwe, jengo hilo halijawahi kukarabatiwa, jambo lililosababisha uchakavu mkubwa wa jengo zima na miundombinu ya ndani, na hivyo kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Bw. Hamis ameongeza kuwa kukamilika kwa ukarabati huo kutakuwa ni faraja kwa wakazi wa Wilaya jirani ambao hutegemea huduma za maktaba hiyo kwa ajili ya kusoma vitabu, hasa watoto wanaohitaji nyenzo za kielimu kama vile hadithi na historia za watu mashuhuri. 

Ukarabati huu unatarajiwa kuleta mwamko mpya wa elimu na kujifunza miongoni mwa wakazi wa Pemba.
Mratibu wa Bodi ya Maktaba Pemba Bw. Ahmed Hamis ( mwenye tisheti) akielekeza kitu kwa Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA Bw. Masozi Nyirenda, wakati wa ziara ya kukagua hali ya uchakavu wa jengo litakalofanyiwa ukarabati.
Muonekano wa hali ya uchakavu katika jengo la Bodi ya Maktaba - Pemba ambalo litafanyiwa ukarabati kupitia TEA

Mratibu wa Bodi ya Maktaba Pemba Bw. Ahmed Hamis ( mwenye tisheti) akielekeza kitu kwa Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA Bw. Masozi Nyirenda, wakati wa ziara ya kukagua hali ya uchakavu wa jengo litakalofanyiwa ukarabati.



Muonekano wa hali ya uchakavu katika jengo la Bodi ya Maktaba - Pemba ambalo litafanyiwa ukarabati kupitia TEA




Ukaguzi wa jengo la Bodi ya Maktaba Pemba ukiendelea kuona hali halisi ya uchakavu kabla ya ukarabati kuanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...