Benki ya Absa kwa kushirikiana na klabu ya The Runners wamekabidhi msaada wa vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja, hususan katika wodi ya wazazi na dharura, ikiwa ni sehemu ya juhudi zao za kuchangia sekta ya afya nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Makamu wa Rais wa The Runners, Godfrey Mwangungulu alisema kuwa huu ni mwaka wa sita mfululizo kwa taasisi hiyo kutoa msaada katika kituo hicho, ambapo lengo kuu ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya, hasa kwa mama wajawazito na huduma za dharura.
Kwa upande wake, Meneja wa Masuala Endelevu na Matukio kutoka Absa Bank Tanzania, Abigail Lukuvi, alieleza kuwa benki hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa The Runners kuhakikisha jamii inapata huduma stahiki. Aliongeza kuwa, sanjari na utoaji wa vifaa hivyo, pia wanachangia damu kwa ajili ya kuimarisha afya za wagonjwa wenye uhitaji.
Akitoa shukrani kwa niaba ya kituo hicho, Dkt. Linda Mutasa, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma kwa akina mama na wagonjwa wa dharura.
Msaada huo wa vifaa tiba umetokana na fedha zilizokusanywa kupitia mbio za hisani zilizopewa jina la Dar City Marathon, ambazo zililenga kuhamasisha umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali, hasa yasiyoambukiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...