Kampuni ya ununuzi wa Tumbaku nchini ya Alliance one imekuja na zoezi la la kuwazadia Pikipiki Wakulima wake wanaopatikana kwa bahati nasibu inayochezwa na Kampuni hiyo kwa Wakulima waliokidhi vigezo katika soko la msimu huu.
Katika msimu huu, Kampuni ya Alliance one inatoa Pikipiki 60 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 168 kwa Wakulima walioingia mkataba nao kutoka mikoa ya kitumbaku ya Kahama, Tabora, Sikonge, Urambo, Kaliua na Kasulu.
Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti amesema lengo kubwa la bahati nasibu hiyo ni kuwahamasisha Wakulima kuweza kupeleka tumbaku yao mapema sokoni ikiwa na ubora na kwamba katika droo ya kwanza waliokidhi vigezo ni wale waliopeleka mapema Tumbaku yao kwa zaidi ya asilimia 30.
“Droo ya kwanza walishinda Wakulima kumi kati ya 1,500 na droo ya pili walishinda Wakulima 12 kati ya 3,214 waliokidhi vigezo vya kupeleka Tumbaku yao mapema sokoni na kwa zaidi ya asilimia 50 ya Tumbaku yote waliyozalisha”.Alisema Wakili Magoti
Ameeleza kuwa Droo ya Tatu iliyofanyikia Urambo jumla ya Washindi 13 kati ya 2,187 wametangazwa, ambapo Kahama wameshinda wawili, Kasulu wawili, Sikonge watatu, Tabora watatu na mkoa wa kitumbaku wa Urambo/ Kaliua wameshinda Wakulima watatu.
Akikabidhi Pikipiki hizo kwa Washindi, Mbunge wa Ushetu na Mdau mkubwa wa Tumbaku kutoka Kahama Emmanuel Charahani ameipongeza Kampuni ya Alliance one kwa kuendesha Bahati nasibu hiyo ambayo imeleta hamasa kubwa kwa Wakulima kuzalisha Tumbaku bora, kuitunza vizuri na kuipeleka sokoni mapema.
Ameielezea Alliance one kuwa ni Kampuni iliyojijengea heshima kubwa kwa Wakulima kutokana na kutoa huduma bora, kwa wakati na yenye kujali ustawi wa mkulima, na kwamba ushirikiano huo umejengwa katika misingi ya uwazi, uaminifu na Bahati nasibu hii imedhihirisha ukweli huo.
Charahani amewaasa Wakulima wa Tumbaku kutojihusisha na utoroshaji ama kuchepusha Tumbaku yao, kwani kufanya hivyo kunadhoofisha hadi kuua vyama vya msingi vya Wakulima kutokana na mzigo mkubwa wa madeni yasiyolipika na kwamba vitendo hivyo vinahatarisha malipo yao binafsi na kuvuruga uwezo wa vyama vya msingi.
“Wito wangu kwenu viongozi wa vyama vya msingi(AMCOS) mjikite kwenye uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa fedha, tabia ya kukopa kupita kiasi na matumizi mabaya ya fedha za Wakulima inachangia kusambaratika kwa baadhi ya Vyama na kuchelewesha malipo kwa Wakulima” ameonya Charahani.
Amewasihii Wakulima kujihadhari na Madalali na Wanunuzi wasioidhinishwa, ambao wananunua Tumbaku yao kwa bei ya chini na kuwanyonya jasho lao kwa manufaa yao binafsi, pia amewataka wauze Tumbaku yao kwa wanunuzi halali ili wawe na uhakika na kipato chao.
“Wito wangu kwa vyombo vya ulinzi na usalama hasa Kahama kushirikiana kwa karibu na Kampuni zilizoidhinishwa katika kudhibiti biashara haramu ya Tumbaku vijijini, hatutaki kuona mazao ya Wakulima yakihujumiwa na Watu wasio na vibali” alisisitiza Charahani.
Mbunge huyo wa Ushetu na mmoja wa Wakulima wa Tumbaku amewataka Wakulima wenzake kuzingatia wajibu wao wa kutunza mazingira kwa mujibu wa sheria ambayo inamtaka kila Mkulima kupanda miti kila msimu ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa kuni kwa ajili ya kukaushia Tumbaku.
Ameipongeza Kampuni ya Alliance one kwa mchango wao mkubwa katika kutunza mazingira kwa kuwa na mashamba ya miti katika maeneo wanayonunua Tumbaku kwa ajili ya kuni za kukaushia na kwamba mpaka sasa wamepanda jumla ya hekta 2,160 katika wilaya ya Kasulu Kigoma na Ngukumo wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Kwa upande wao baadhi ya Wakulima waliozawadiwa Pikipiki baada ya kushinda katika droo hizo Edward Zunzu, Elizabeth Mayunga na Ramadhan Iddi wamesema Kampuni hiyo imewaongea ari ya kuzalisha, kutunza kwa ubora na kuwaisha sokoni Tumbaku zao kwa misimu mingine na kuwataka Wakulima wenzao kuzingatia kanuni bora za kilimo na utunzaji wa Tumbaku.
"Mimi sikutegemea kushinda pikipiki hii kwa sababu sisi ni wachache mno ikilinganishwa na idadi kubwa ya Wakulima waliokidhi vigezo vya kuingia kwenye droo kwakweli ujanja ni kuwahisha zao mnadani kutoka huko mashambanj shambani," alisema Elizabeth Mayunga.
"Mimi nawasihi wakulima wenzangu kutokata tama na kwamba kila hatua imefanyika kwa uwazi na sisi tumeshuhudia hapa leo," amesema Rashid Iddi.
Edward Zunzu amesema "Mimi naenda kuwa balozi wa kampuni hii huko kwetu nikawahimize wakulima umuhimu wa kuwahisha mazao sokoni na mwakani ninyi mtaona mbio zake zitakavyokuwa."Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani akimkabidhi Mkulima Ramadhan Iddi kutoka Sikonge, ambaye ni mmoja washindi wa pikipiki zilitolewa na kampuni ya Alliance One kwa kuwahisha tumbaku sokoni katika hafla iliyofanyika ofisi za Alliance One wilayani Urambo mkoani Tabora.
Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani(mbele katikati),Mkurugenzi wa Kampuni ya Alliance One Mathew Zembe(Mbele Kulia) na Msemaji wa kampuni hiyo John Magoti(Mbele Kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wakulima waliosimama nyuma yao, ambao ni washindi wa pikipiki 10 kati ya 60 zilizotolewa na kampuni ya Alliance One kwa kuwahisha tumbaku sokoni.Hafla hiyo ilifanyika ofisi za Alliance One wilayani Urambo mkoani Tabora.
Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani akimkabidhi Mkulima Elizabeth Mayunga kutoka Sikonge ambaye ni mmoja washindi wa pikipiki zilitolewa na kampuni ya Alliance One kwa kuwahisha tumbaku sokoni katika hafla iliyofanyika ofisi za Alliance One wilayani Urambo mkoani Tabora.
Mgeni rasmi akiwasili na kuweka saini kwenye kitabu cha wageni
Mgeni rasmi akipata mawili matatu kutoka kwa Msemaji wa Kampuni
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...