Kwa kauli moja leo tarehe 13 Mei 2025 Bunge la Tanzania limepitisha kwa kishindo bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi zake kwa mwaka 2025/2026 yenye jumla ya shilingi Trilioni 2.439.

Bajeti hiyo imepitishwa kwa asilimia 100 na wabunge ili kuwezesha utekelezaji wa malengo yaliyoanishwa kwa mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi zake.

Kati ya fedha hizo zilizopitishwa jumla ya shilingi Bilioni 688.6 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara ambapo Shilingi Bilioni 635.2 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi Bilioni 53.3 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.

Utekelezaji wa bajeti hiyo utajikita zaidi katika maeneo matano ya vipaumbele ambayo ni i) kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya sheria, Uandaaji wa miongozo, na utoaji wa mafunzo, ii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya Amali katika shule za sekondari na vyuo vya Amali, iii) Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya Amali, Msingi, Sekondari na Ualimu, iv) Kuongeza na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na v) Kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, Matumizi ya Sanyansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Wabunge wamempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda (Mb) kwa utulivu wa kiutendaji katika wizara yake na mshikamano alionao na watendaji wote wa Wizara na kumsihi kusimamia kwa weledi mkubwa wizara hiyo ambayo ni msingi wa maendeleo ya nchi.

Kati ya fedha zilizopitishwa, zaidi ya shilingi Trilioni 1.7 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 1.186 ni fedha za ndani na Shilingi 560.8 ni fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imeidhinishiwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.2 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Mishahara ni Shilingi Bilioni 1.5 na Matumizi Mengineyo ni Shilingi Bilioni 1.7

Waziri Mkenda amesema kuwa jumla ya wabunge 36 wamechangia moja kwa moja huku wengine wakichangia kwa maandishi ambapo wote kwa pamoja wameshauri na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa ya pili ya elimu sambamba na ongezeko kubwa la bajeti.

Pia Waziri Mkenda amesema kuwa wabunge wote waliochangia pia wamempongeza Rais Samia kwa kuongeza mikopo elimu ya juu, ongezeko la Vyuo vya Ufundi stadi-VETA, Ujenzi na ongezeko la shule za Amali pamoja na Ujenzi wa kampasi mpya za vyuo vikuu.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...