Imeelezwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko tarehe 2 Juni 2025 atazindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.


Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema uzinduzi wa Mkakati utaenda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na  Uelimishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


Mramba ameeleza kuwa mkakati huo umeandaliwa na Wizara ya Nishati  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), ikiwa ni pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


 Ameongeza kuwa  uzinduzi huo utaenda sambamba na Wizara ya Nishati  kukabidhiwa magari mawili kwa ajili ya  kuendesha Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuwafikia wananchi hasa sehemu za vijijini.


Mhandisi Mramba amesema Mkakati unalenga masuala mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za nishati safi ya kupikia katika afya, mazingira na uchumi wa kaya, kuhamasisha mabadiliko ya tabia kutoka kwa matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kama mkaa na kuni, kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika soko la bidhaa za nishati safi ya kupikia na kujenga mazingira ya sera na udhibiti yanayosaidia upatikanaji na upatikanaji wa nishati safi kwa wote.


Amesema mbinu mbalimbali za mawasiliano zitatumika  ikiwemo  vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa,  viongozi wa kimila, kidini, na kisiasa, matumizi ya mitandao ya kijamii na mafunzo kwa watendaji wa Serikali na Waandishi wa Habari na kuyafikia makundi mbalimbali  ya wananchi wa mijini na vijijini, wanawake na vijana, watoa huduma za afya, viongozi wa serikali za mitaa, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.


Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa  Umoja wa Ulaya upande wa Tanzania na Bw. Immanuel Muro, Mtaalam Mwandamizi wa fedha kutoka UNCDF ambao kwa pamoja wameeleza kuunga mkono juhudi za Serikali katika Uhamasishaji wa Nishati Safi ya Kupikia.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...