Katika jitihada za kuimarisha ustawi wa wananchi wa Kata ya Mjini Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, Diwani Mathew Ngalimanayo amesema serikali imepiga hatua kubwa katika kuboresha maisha ya wakazi kupitia maboresho ya miundombinu na uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi mbalimbali.
Akiwa katika ziara ya kukutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mitaa yote minne ya kata hiyo leo Mei 28, 2025, amefika katika mtaa wa Mahenge na Mashujaa, Ngalimanayo ameeleza kuwa serikali imefanikiwa kujenga madaraja matatu imara ambayo ni daraja la Upendo, lililopo makaburini Mahenge na linalounganisha Mahenge A na Kimoro, ambayo yameongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Aidha, barabara zote za ndani ya Kata ya Mjini sasa zimetambuliwa rasmi na kuingizwa katika mfumo wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua inayoweka msingi wa matengenezo endelevu na uendelezaji wa miundombinu hiyo kwa viwango vinavyohitajika.
Katika nyanja ya maendeleo ya kiuchumi, Ngalimanayo amesema kuwa zaidi ya vikundi 100 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vimesajiliwa rasmi, na ni miongoni mwa vikundi vitakavyonufaika na mikopo ya Halmashauri, na mikakati ya kupata Mafunzo ya ujasiriamali pia ili kuongeza ufanisi wa wanavikundi hao katika kutengeneza bidhaa na kuendesha biashara.
Katika sekta ya barabara, Diwani ametaja mafanikio ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zinazojumuisha njia ya SOUWASA kuelekea kwa Swai, kutoka Kanisa la Sabato hadi Kanisa la Anglikana, kutoka Kituo cha Azam hadi Msikiti Mpya, na kutoka Huduma Klabu hadi Shinyanga Guest House kupitia Hoteli ya Parokia.
Kwa upande wa kisiasa, amesisitiza mshikamano ndani ya CCM na jumuiya zake kwa kuendeleza michango, uratibu wa shughuli za chama, na kusaidia wanachama wanaokumbwa na changamoto mbalimbali, amepongeza uongozi wa Rais Samia na Mbunge wa Jimbo la Songea kwa ushirikiano unaoimarisha maendeleo ya Kata ya Mjini.
Kwa mujibu wa Ngalimanayo, dhamira kuu ni kuleta maendeleo endelevu kwa kushirikiana na wananchi katika misingi ya uwazi, uwajibikaji na mshikamano.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...