Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Vitta Rashid Kawawa, amekabidhi dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 14.5 kwa Zahanati ya Luangano, iliyopo Kata ya Mputa, Wilayani Namtumbo. Makabidhiano hayo yalifanyika rasmi tarehe 9 Mei 2025 katika viwanja vya zahanati hiyo.
Zahanati ya Luangano imejengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na mbunge wao, ambaye alichangia shilingi milioni 5 kwa ajili ya ujenzi. Wananchi walitoa eneo, wakatengeneza matofali, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi hadi mradi huo kukamilika na kuanza kutoa huduma.
Uzinduzi wa zahanati hiyo umeleta matumaini kwa wakazi wa kijiji hicho waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya. Sasa, huduma zitapatikana karibu na makazi yao, jambo linalotarajiwa kupunguza vifo na madhara yanayosababishwa na kuchelewa kupata matibabu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Luangano, Kawawa aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Kata ya Mputa, ikiwemo sekta ya afya.
“Zahanati hii itanufaisha watu wote – kina mama, watoto, wazee na kila mkazi wa kijiji hiki. Ni matokeo ya nguvu ya pamoja. Leo nimewaletea dawa na vifaa tiba, na ninaikabidhi rasmi zahanati hii kwenu,” alisema Kawawa. Aliongeza kuwa kuna zahanati nyingine zinazoendelea kujengwa, ikiwemo jengo la mama na mtoto Naikesi, na maboresho mengine katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.
Mbunge huyo aliwataka wananchi waendelee kumuunga mkono na kumpa nafasi nyingine katika uchaguzi wa Oktoba 2025 ili aweze kuendeleza jitihada za kuwaletea maendeleo. “Mimi ni mtumishi wenu. Bungeni huwasilisha mahitaji ya wananchi kwa heshima na maelewano. Miradi hii inadhihirisha matokeo ya utumishi huo,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, Dkt. Aaroon Hyera, alisema Zahanati ya Luangano ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na Kawawa katika kuboresha huduma za afya wilayani humo. “Tuna magari matatu ya wagonjwa kwa sasa, jambo ambalo halikuwepo kabla ya uongozi wake. Bila Kawawa, hatungefika hapa,” alisisitiza.
Naye Diwani wa Kata ya Mputa, Swalehe Said Motto, alisema wananchi hawana deni kwa mbunge wao, bali wao ndio wenye deni la kumlipa kwa maendeleo aliyowaletea katika sekta za elimu, afya na maji. Pia walimkumbusha kuhusu umuhimu wa kuharakisha upatikanaji wa umeme ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Namtumbo, Ndg. Katobes, kimempongeza Kawawa kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya CCM, hususan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na makazi yao.
Mbali na dawa na vifaa tiba, Kawawa pia alikabidhi mabomba na vifaa vya kuunganishia huduma ya maji kwa zahanati hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...