*Asema atataka atakayevuruma amani achukuliwe hatua
*Azindua soko la nyama choma la Vingunguti jijini Dar
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa amesema kwamba Tanzania haitamvumilia mtu yoyote kutoka ndani na nje ya nchi anavuruga amani iliyopo huku akitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wote nchini kuhakikisha wanasimamia kikamilifu amani ya taifa hili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akizindua Soko la Nyama choma la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lililopewa jina la Kumbilamoto lililopo Kata ya Vingunguti,Mchengerwa ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa amani.
“Tutailinda amani ya nchi hii kwa nguvu zetu zote. Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndiyo wenye viti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao.Lindeni mipaka ya maeneo yenu . Wadhibitini bila kurudi nyuma,”amesema Mchengerwa.
Amefafanua kuwa Tanzania ilirithishwa amani na waasisi wake na dhamira ni kurithisha amani hiyo kwa vizazi vijavyo, hivyo kwa yule asiye sikia na anajipanga kuvuruga amani wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya washughuke naye haraka.
Ametoa mfano kuwa wanaofanya vurugu katika Mkoa wa Dar es Salaam, siyo wakazi wa mkoa huo bali wanatoka mikoani na nje ya nchi.“Wadhibiti bila kurudi nyuma.Lindeni mipaka ya maeneo yenu,”amesisitiza.
Kuhusu uzinduzi wa soko hilo , Waziri Mchengerwa ametoa pongezi kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala kwa kasi kubwa ya maendeleo, ukiwemo ubinifu wa miradi hiyo na ukusanyaji mapato.
" Soko la Nyama Choma la Kumbilamoto ni fursa kubwa katika jamii kwani linachochea kipato cha wafanyabiashara na serikali,"amesema Waziri Mchengerwa ambaye kabla ya kuzindua soko hilo alipata nafasi ya kuzungumza na baba na mama lishe ambao waliiopongeza Serikali chini ya Rais DK.Samia Suluhu Hassan kuwajali wananchi.
Wakati huo huo huo Waziri Mchengerwa amemkabidhi gari Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto na kushuhudia utiwaji saini mikataba sita ya ujenzi wa barabara za lami wilayani Ilala.
Akizungumzia mikataba sita ya ujenzi wa barabara iliyotiwa sani Mchengerwa ameeleza ni dhamira ya Rais Dk. Samia kuona barabara hizo zinajengwa na kuwaondolea kero ya usafiri wananchi, kuimarisha mifumo ya kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkoa huo uko salama na wanaendelea kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani .
Wakati huo huo Naibu Spika wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam Mussa Azzan ‘Zungu’ amewaonya wana siasa ambao ni wabunge au waliwahi kuwa wabunge wanaojaribu kutumia njia za uvunjifu wa amani na kumsema vibaya Rais Dk. Samia.
“Hii inatusikitisha. Wanajua taratibu na njia sahihi za kuchukua.Ni wabunge au waliwahi kuwa wabunge. Njia sahihi ni mazungumzo. Waje tukae nao tuzungumze,”alisema Zungu.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alimhakikishia waziri huyo, wilaya hiyo itaendelea kuchapa kazi kuhakikisha miradi yenye tija katika jamii inatekelezwa na kunufaisha wananchi.
Awali Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amezungumza kuhusu umuhimu wa soko hilo na kusisitiza ni maalumu kwa wachomaji nyama, mama na babalishe wa vingunguti
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...