Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKE wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb, ametoa rai kwa viongozi nchini kuhakikisha wanafanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli na si kwa dhana au hisia kwani hivi sasa kumekuwa na taarifa potofu na zenye upotoshaji mkubwa.
Ametoa rai hiyo leo Mei 16,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya Nane ya Taasisi ya Uongozi ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea uwepo wa madhara ya taarifa potofu na upotoshaji.
“Viongozi wanapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli na si kwa dhana au hisia.Kama viongozi, ni lazima kuhakikisha hawafanyi maamuzi yatakayowaumiza wananchi.
“Nawahimiza wote kuhakikisha mnachangia kwa namna yenye maana katika maendeleo ya Tanzania,” amesema na kutoa pongezi kwa Taasisi ya Uongozi kwa kuanzisha programu ya uongozi kwa wanawake.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ametumia mahafali hayo kukumbusha umuhimu wa kufanyia marekebisho mchakato wa kuwathibitisha Wakurugenzi Wakuu ili kuepusha migogoro kazini.
Amesema uzoefu umeonyesha viongozi wengi wamejikuta wakikumbwa na migogoro licha ya kufanya kazi kwa ufanisi huku akitoa mwito kwa viongozi kubuni mbinu madhubuti za kuratibu utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali fedha na watu katika kuleta matokeo chanya na yenye tija.
“Kama mnavyofahamu, serikali inafanya uwekezaji mkubwa wa kifedha kwenye miradi hii ili kuchochea maendeleo ya taifa na kuboresha maisha ya wananchi wetu,” amesema Waziri Simbachawene.
Aidha amesema amesema amefahamishwa Taasisi ya UONGOZI ina wakufunzi wa kitaifa na kimataifa na waliobobea kwenye masuala ya uongozi na maendeleo endelevu.
“Naamini kabisa kuwa wawezeshaji hawa watakidhi matarajio yenu na mtakapomaliza mtatoa ushuhuda juu ya hili kama mlivyosikia katika hotuba ya wenzenu waliotukutanisha hapa kusherekea mafanikio haya makubwa.
“Nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo, Umoja wa Ulaya na UN Women kwa kufadhili Programu ya Uongozi kwa Wanawake, na Serikali ya Finland kwa kuendelea kufadhili programu za mafunzo ya uongozi pamoja na shuguli nyingine za Taasisi.
“Utayari wenu katika kuendelea kufadhili program hizi unaonesha namna ambavyo mnashiriki kuwezesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia malengo yake kwa kuwa na Viongozi wenye sifa, weledi na uwezo wa kusimamia shughuli za maendeleo ya nchi.”
Wakati huo huo Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, ameeleza kwamba uongozi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya nchi.Timu bora huundwa kwa watu mbalimbali wenye utofauti.“Ni wakati muafaka kutumia muda wetu mwingi kufanikisha mafanikio bora.”
Kwa upande wake Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Juhana Lehtinen, amesema kuwa Taasisi ya Uongozi ni historia ya ushirikiano kati ya Finland na Tanzania.
“Tunaona fahari kuwa sehemu ya uongozi wa ndoto na wenye maono wa Taasisi ya Uongozi. Kwa miaka yote taasisi hii imekuwa maarufu duniani,” amesema na kusisitiza serikali yao itaendelea kuunga mkono Taasisi ya Uongozi.
Akizungumza katika mahafali hayo Katibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, awakumbusha viongozi kutumia ujuzi walioupata kuwahamasisha wengine na kuchangia maendeleo yenye maana.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, amesema tukio hilo limeandaliwa kusherehekea mafanikio ya waliokamilisha programu za muda mrefu za taasisi hiyo: Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (PGD), Cheti cha Uongozi (CiL), na Mpango wa Uongozi wa Wanawake (WLP).
“Zaidi ya viongozi 200 wamehitimu katika programu hizo tatu, ambazo zimehudhuriwa na viongozi kutoka bara zima – na kutoka sekta mbalimbali kama serikali, biashara, elimu ya juu na asasi za kiraia.”





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...