Wahitimu wa Vyuo mbalimbali wametakiwa kuepuka kutumiwa na baadhi ya vyama vya siasa kujiingiza kwenye maandamano yakuleta uchochezi yanayolenga kupelekea uvunjifu wa amani ya nchi kwani wakipata changamoto ni hasara kwao na familia zao.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha mapinduzi Taifa Mkoa wa Ruvuma MNEC Hemed Challe, akiwa mgeni rasmi kwenye Mahafali ya Seneti ya Vyuo Mkoani Ruvuma kupitia CCM, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha ualimu Songea.
Amesema kumekuwa na wimbi la vijana ambao wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya vyama vya siasa kuleta uchochezi hivyo wasikubali kupotoshwa kuingia katika makundi yakuondoa amani kwa taifa na ikitokea changamoto yoyote Ile vyama hivyo havitawasaidia na badala yake watakwenda kuwapa mizigo wazazi wao.
Amesema wazazi wamepambana kuhakikisha wanawasomesha ili baadae waje kunufaika na matunda ya uwekezaji wao hivyo waondoke wakijua wanajukumu la kuwasaidia wazazi na familia zao na wawe mabalozi wakutangaza umoja na mshikamano kwa Watanzania wote.
Amewataka kwenda kuitumia vizuri elimu waliyoipata ili kutoa mchango kwenye ujenzi wa Taifa na kila mmoja anajukumu la kuhakikisha Tanzania inakuwa kitu kimoja kwani tayari wamepata elimu ya Chama na elimu ya kitaaluma hivyo elimu hizo zikachochee uzalendo kwa taifa.
Akizungumzia uchaguzi Mkuu wa mwaka huu MNEC Hemed, amewataka waende kukisaidia Chama kwa kuwapa elimu Watanzania kushiriki uchaguzi bila machafuko ilikiendelee kushika dola kwani umoja na mshikamano ni tunu muhimu katika kulinda amani ya nchi.
Amewaasa kuendelea kukitumikia Chama hicjo kwani hakijawahi kumsahau mtu jambo muhimu ni kuendelea kuwa na uvumilivu, utiifu na uadilifu kwani wahitimu wote wa seneti taarifa zao zinaingizwa kwenye kumbukumbu muhimu na kukiwa na fursa hupewa kipaumbele kutokana na nidhamu waliyonayo.
Akieleza kuhusiana na namna ya kukabiliana na changamoto za ajira nchini, amewataka wahitimu hao kwenda kuanzisha vikundi mbalimbali kwenye maeneo yao na kutumia fursa za mikopo ya Halmashauri kwa kubuni mradi utakao waingizia kipato kipindi ambacho wanasubiri kuajiriwa.
Akisoma Risala ya Wahitimu Rose Abraham Challe ambae ni muhimu wa Seneti, amesema wao kama wasomi watazidi kukipigania Chama kwani wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata mafunzo, kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, pamoja na kuwasajili wanachama vyuoni kwa mfumo wa kielektroniki.
Ametoa pongezi kwa Seneti Mkoa wa Ruvuma uongozi wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma, na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Kazi anazozifanya ili kukiletea Chama maendeleo, huku akiomba kuwezeshwa zaidi ili kuendelea kupata mafunzo na semina.
Mahafali ya Seneti ya Vyuo Mkoani Ruvuma kwa mwakka 2025, imefanyika katika Chuo cha Ualimu Songea na kuhusisha vyuo mbalimbali ikiwemo Veta Msamala, St Thomas, Skaite, Chuo cha Ualimu Songea, na zaidi ya wahitimu 200 wamehitimu, na ahadi yao ni kuhakikisha vyuo vyote 44 ndani ya Mkoa huu itatawala rangi ya kijani na njano na kura zote zitakuwa kwa Rais Samia na watahamasisha jamii kushiriki uchaguzi Mkuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...