Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kinatarajia kujenga hospitali ya kisasa ya moyo kupitia Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu Afrika Mashariki huku Uzinduzi wa mradi huo ukinatarajiwa kufanyika Mei 23, mwaka huu katika Kampasi ya Mloganzila.


Akizungumza na vyombo vya habari Leo Mei 19,2025 jijini Dar es Salaam , Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema ujenzi huo ni sehemu ya mpango mkakati wa MUHAS katika kuboresha huduma za afya ya moyo kwa wananchi wa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.


“Awamu ya pili ya mradi huu imelenga kujenga hospitali ya kisasa ya moyo, kuendeleza mitaala ya kitaalamu, kufanya tafiti za kina kuhusu kinga, tiba na ukarabati wa magonjwa ya moyo, pamoja na kuanzisha programu za kijamii kwa ajili ya uhamasishaji wa afya ya moyo,” amesema Profesa Kamuhabwa.


Amesisitiza kuwa Awamu ya Kwanza ya mradi huo tayari imekamilika kwa mafanikio makubwa, na ilijumuisha ujenzi wa jengo la kufundishia (Multipurpose Building) na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu wa afya kutoka ndani na nje ya nchi.


Katika kuelekea uzinduzi wa awamu hiyo mpya, MUHAS imeandaa Kambi Maalum ya Afya ya Moyo kwa wananchi, itakayofanyika kwa siku mbili yaani Mei 21na 22, mwaka huu kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, katika Kampasi ya Mloganzila.


“Kambi hii itatoa huduma ya bure kwa wananchi wote, ikiwemo uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, uchunguzi wa visababishi vyake, elimu na ushauri wa kiafya, matumizi sahihi ya dawa za moyo, pamoja na huduma saidizi kwa wagonjwa wa moyo,” amesema Profesa Kamuhabwa.


Ameongeza,"Pia wananchi  watapata fursa ya kujionea bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa MUHAS, ikiwa ni sehemu ya maonesho ya kitaaluma na ubunifu wa chuo hicho,"


Profesa Kamuhabwa amewataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hiyo ya afya ili kushuhudia uzinduzi wa hatua hiyo muhimu katika historia ya huduma za afya nchini.


Kauli mbiu ya tukio hilo ni 'Linda Afya ya Moyo Wako' ikiwa imelenga kuhimiza jamii kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa ya moyo, ambayo yameendelea kuongezeka kwa kasi nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...