Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amezungumza hayo mara baada ya
kubadilisha taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo
cha Ofisi ya Mtendaji wa kata Kilimani, Jijini Dodoma, tarehe 16 Mei, 2025.
"Nimekuja hapa kwenye kituo cha kujiandikisha kwenye
daftari la kudumu la wapiga kura nimepata huduma nzuri sana, na ndani ya muda
mfupi wamenitengenezea kadi nzuri ya kisasa na yakidigital."
Mhe. Johari amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi
kushiriki katika zoezi hilo ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba na
kujiandikisha kwa ajili ya kuchagua viongozi mbalimbali kwa mujibu wa sheria na
katiba, pia amesema zoezi hilo la kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura
linachukua muda mfupi mpaka kukamilika kwake.
"Nichukue fursa hii kuwaasa wananchi wajitokeze kwa
wingi kushiriki katika zoezi hili, kwani zoezi lenyewe linachukua muda mfupi
wanahakiki taarifa zako na unapata kitambulisho chako kwa haraka".
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutumia mifumo ya kisasa na
kuandaa utaratibu mzuri unaowaruhusu wananchi kujiandikisha na kuhakiki taarifa
zao kwenye daftari la wapiga kura katika muda mfupi.
"Niwapongeze Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi
nzuri wanayoifanya kwani utaratibu ni mzuri na huduma hii inatolewa kwa haraka
sana".
Zoezi la kujiandikisha na kuhakikisha taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Dodoma limeanza tarehe 16 Mei, 2025 litaendelea hadi tarehe 22 Mei, 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...