Tunduru-Ruvuma.
Makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Namtumbo kwenda Wilaya ya Tunduru yamefanyika leo Mei 16, 2025 katika eneo la Mpakate Wilayani Tunduru, makabidhiano hayo yamefanywa kati ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Namtumbo umekimbizwa umbali wa kilomita 311 na umetembelea miradi 10 ya maendeleo, baadhi ikizinduliwa na mingine kukaguliwa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ussi, amesifu mapokezi mazuri ya wananchi wa Namtumbo na juhudi zao katika kuenzi misingi ya Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni pamoja na usimamizi bora wa miradi ya maendeleo ameongeza kuwa mwitikio wa wananchi kwenye kila mradi uliotembelewa umeonyesha mshikamano amani na matumaini makubwa kwa Taifa.
Ismail Ussi pia amewasihi wananchi kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa amani, huku akieleza kuwa Mwenge wa Uhuru umeacha alama ya utulivu na mshikamano katika maeneo yote waliyopita, ametoa shukrani kwa viongozi wa serikali na chama cha Mapinduzi kwa ushirikiano mzuri, na kuwataka waendelee kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea uchaguzi wa Oktoba 2025.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utapita katika miradi 11 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.2. Mwenge huo utatembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi hiyo, na utakimbizwa kwa zaidi ya kilomita 100 ndani ya wilaya hiyo hadi eneo la mkesha.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukesha Tunduru kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa Mkoa wa Mtwara kesho asubuhi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...