Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo  imenunua na kuipatia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ndege moja ya kisasa kwaajili ya kupambana na visumbufu vya mimea ikiwemo kwereakwerea na nzige huku Serikali ikitenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kwaajili ya kununua ndege zingine tatu za kisasa kusaidia wakulima kupambana na majanga hayo nchini.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) akikagua na kupata maelezo ya ndege hiyo kutoka kwa rubani aliyeisafirisha kutoka nchini Marekani hadi Tanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) kwenye hafla ya kupokea ndege hiyo ya kisasa aina ya THRUSH 510P2­­+  iliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na mshirika yasiyo ya kiserikali, Wabunge, wandau wa maendeleo ya Kilimo na  Wananchi.

“ Hivi sasa tuna takribani hekta laki tisa za umwagiliaji nchi nzima na tunataabika, lakini tunafikiria kufikia hekta milioni 3 au 5  naamini utakuwa mtihani mkubwa hivyo ni lazima tujiandae, Kwahiyo maelekezo yangu kwa TPHPA na Mwenyekiti wa bodi na katibu Mkuu wa Wizara ni kwamba, Mchakato ule tulioupitia wa miaka miwili wa kununua ndege hii ya kwanza sitaki tuurudie tena”. Alisisitiza Mhe. Bashe.

Aliongeza “ Kwakuwa kwenye bajeti ijayo tumepitisha kunzisha vituo vinne vya kilimo Anga kwa maana ya Arusha, Mbeya pale Songwe Airpot na Mwanza Vituo hivi vyote vinatakiwa kuwa na ndege na ndege zisizo na rubani (DRONES)  kwahiyo naagiza mchakato wa kununua ndege zingine tatu kama hii ya leo uanze mara moja maana ni lazima kama nchi tujitegemee maana dunia ya kubebana haipo, lakini niwashukuru sana Shirika la Chakula Duniani (FAO) wamesaidia sana kuiboresha TPHPA kufanikisha kuwa na vutuo 36 kwenye mipaka yetu ambavyo vitakuwa na vifaa na maabara za kisasa”.

Aisha Mhe. Bashe amesema wamefanikiwa kununua droni kwaajili ya kufanya ufuatiliaji na mwaka huu wanatarajia kuongeza zingine za kisasa kwaajili ya kufanyakazi ya kupulizi viautilifu kwenye mazao lakini amewataka watanzania kutambua kuwa Tanzania imepata bahati mbaya  ya kuwa na maumbile ya mazalia ya Nzige kwenye mikoa ya  Dodoma, Katavi na Rukwa na kwa bahati mbaya ni Nzige wekundu.

Waziri huyo wa kilimo amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuanza mchakato wa kuongea na Mamlaka ya Viwanja vya ndege nchini kuwapatia maeneo kwenye viwanja hivyo kwaajili ya kujenga vituo vya Mamlaka ya afya ya mimea kwenye viwanja hivyo na kuweka vifaa vyote muhimu kwenye kanda zote nne kila kanda iwe na ndege yake na vifaa vyake kwaajili ya kupambana na majanga ya wadudu hao hatari wanashambilia mazao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof.Joseph Ndunguru ameseama ujio wa ndege hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini hasa kwa wakulima wa maeneo ya Bahi Dodoma, Kondoa Singida, Mvomero na Kilosa Mkoani Morogoro,Mbarali na Kapunga Mkoani Mbeya,Ruvu Mkoani Pwani, Simiyu,  Mara na maeneo mengine mengi ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za nzige na kwelea kwelea na kuwapa wakulima hasara kubwa.

“Udhibiti wa ndege hao kwa miaka yote tumekuwa tukitumia ndege ya kukodi ya Shirika la udhibiti wa Nzige wa Jangwani (DLCO -EC) kutoa nchini Kenya na hivyo muda mwingine kujikuta tunachelewa kuwasaidia wakulima wetu wanapotuhitaji kwa wakati kutoka na sababu mbalimbali hasa za kiutawala kuhitajika kusubiria foleni yetu ifike kwakuwa ndege hiyo kuwa inatumiwa na nchi mbambilimbali za afrika mashariki, hivyo ujio wake ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wetu” Alibainisha Prof. Joseph Ndunguru.

Aliongeza “Ndege hii unaweza kuiona ni ndogo lakini inauwezo mkubwa sana, kwani ina tenki la mafuta la ujazo wa lita 863 ya kuiwezesha kukaa angani bila kutua kwa zaidi ya masaa manne, lakini pia ina uwezo wa kubeba viuatilifu lita 1930 karibu lita 2000 kwahiyo kuifanya kuwa na uwezo wa kudhibiti ndege hao kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2400 kwa mara moja sambamba na kuwa na vifaa vya kisasa kufanya ufuatiliaji na kutoa takwimu zinazowezesha kufanya mipango ya kuwadhibiti”.

Prof. Ndunguru amesema kuwa kwa kumia ndege hiyo sasa watakuwa na uwezo wa kufikia maeneo mapana kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma walipotumia mbinu za kizamani kuhakikisha kwamba athari za ndege aina ya Kwelea kwelea zinapungua na hivyo kulinda mazao ya wakulima na hatimaye kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa taifa.

Mkurugenzi huyo Mkuu wa TPHPA amesema Halmashauri za wilaya 40 nchini huvamiwa na ndege waharibifu aina ya Kwelea kwelea wanaokadiriwa kufikia milioni 200 kila mwaka wenye uwezo wa kuharibu takribani tani 450,000 za nafaka lakini pia kwa kipindi cha kiangazi skimu za umwagiliaji wa mpunga 38 zimekuwa zikivamiwa na ndege hao wapatao takribani milioni 100 kila mwaka wenye uwezo wa kula na kuharibu karibu tani za mpunga 225,000.

Hivyo Prof. Joseph Ndunguru ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka histosria hii katika kipindi chake cha uongozi wa Serikali ya wamu ya sita kwa kufanya mageuzi makubwa katika mamlaka hiyo ikiwemo kununua ndege hiyo aina ya THRUSH 510P2­­+ kwa gharama za shilingi bilioni 6 za kitanzania ili kusaidia wakulima nchini.

Nae mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Mariamu Ditopile Mzuzuri kwa niaba ya Bunge ameipongea Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru na na watumishi wengine kwa kufanikisha ndoto hiyo ambayo imeotwa kwa muda mrefu.

“Toka tumeanza Bunge kwenye Serikali hii ya awamu ya sita Mhe. Waziri pamoja na timu yako kuna mambo mengi ambayo umekuwa ukija nayo kwenye kamati hizi tunashangaa kwakuwa  ni vitu ambavyo hatujazoea kabisa kwenye kilimo, hata lilipokuja swala la ununuzi wa ndege hii tuliona ni maneno maneno  lakini sasa tunaona fahari kwa kazi hii nzuri na kuzingatia mapendekezo na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Wabunge Bungeni” alisema Mhe. Mzuzuri.

Aliongeza “Kwakweli huu ni ukombozi kwa wakulima wetu maana tumekuwa tukisikia malalamiko mengi kwa wakulima kwenye maeneo mbalimbali kama ambavyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Staki Senyamule alivyosema lakini kumbe ndege tuliyokuwa tunaitumia ni ya kukodi kutoka Kenya na ilikuwa ikitumiwa na nchi zingine pia, hivyo wanafika wanakutana na foleni ya kusubiria wakati wakulima mazao yanazidi kushambuliwa  sasa tumepata ndege yetu wenyewe itakayowakomboa wakulima wetu na kuwafuta machozi ya kuharibiwa kwa mazao yao”.

Kwa upande wake Mweyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya (TPHPA) Prof. Andrew Temu kwa niaba ya wajumbe wa bodi na wafanyakzi wote wa ameahidi kuitunza ndege hiyo na vifaa vyote ambavyo Serikali inavitoa katika kuhakikisha vinafanya kazi iliyokusudiwa kwa maslahi mapana ya taifa sambamba na kutoa mafunzo kwa watumishi namna ya kutumia vifaa hivyo vya kisasa kwa na kupeleka mtu kusomea namna ya kuendesha ndege hiyo na fundi wa kuifanyia matengenezo.

Aidha amesema amepokea maelekezo ya kuanza mchakato wa kununua ndege zingine tatu na kupata moja ya kufanya ufuatiliaji ili kuipa ndege hii iliyopokelewa nafasi ya kufanya kazi kubwa ya kupulizia viuatilifu na kuua wadudu huku akiona fursa ya kutumia kiwanda cha kuunganisha ndege cha Morogoro katika kupata ndege hizo zingine zitakazofuata.

 MATUKIO KATIKA PICHA HAFLA YA UZINDUZI NA UPOKEAJI WA NDEGE HIYO.

 

Ndege hiyo ikipata heshima ya watal saluti mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof.Joseph Ndunguru  akitoa salamu za Mamlaka hiyo na maelezo ya ndege hiyo.

 

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Staki Senyamule akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma.


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Mariamu Ditopile Mzuzuri akitoa salamu za Wabunge.






Mweyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya (TPHPA) Prof. Andrew Temu akitoa salamu na shukrani kwa niaba ya Bodi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...