Benki ya NMB imenunua na kugawa vitanda, madawati, viti na meza vyenye thamani ya Shilingi milioni 125.2 katika shule 15 za Wilaya ya Arusha na Arumeru.
Kati ya shule hizo zilizonufaika, 11 ni za Arusha Jiji ikiwemo shule za msingi Unga Limited waliopewa madawati 150, huku Baraa, Lemara, Sanawari, Elerai na Kijenge kila moja ikipata madawati 100.
Shule zingine ni za sekondari ambazo ni Unga Limited, Elerai, Kimaseki, Osunyai na Salei zilizopokea viti na meza 50 kila moja.
Katika Wilaya ya Arumeru, shule ya Sekondari Oldadai imekabidhiwa vitanda vya ghorofa (double decker) 33, huku Kiutu na Kiserian zikikabidhiwa viti na meza 60 kila moja, na shule ya msingi Mussa ikipokea madawati 50.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, alisema msaada huo una thamani ya Shilingi milioni 125.2.
“Kwa shule za Arusha Jiji, vifaa vina thamani ya Shilingi milioni 88.2, huku vifaa vilivyotolewa kwa shule za Arumeru vikiwa na thamani ya milioni 37. Lengo letu ni kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazokabili jamii yetu, hususan katika sekta ya elimu na afya,” alisema Baraka.
Aliongeza kuwa NMB inatambua jitihada za serikali katika kuboresha elimu na afya, na hivyo benki imekuwa mstari wa mbele kusaidia kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii.
“Tangu miaka 10 iliyopita, tumeweka utaratibu wa kutenga asilimia moja ya faida yetu kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii. Hii ni njia yetu ya kurudisha kwa jamii inayotuwezesha,” aliongeza.
Baraka alibainisha kuwa juhudi hizo zimetambuliwa kimataifa, ambapo jarida la Global Banking & Finance Magazine la Marekani limeitaja NMB kuwa kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii Tanzania kwa mwaka 2025, sambamba na kuitambua kama Benki Salama Zaidi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, aliishukuru NMB kwa msaada huo na kuipongeza kwa kuwa na uelewa wa kina kuhusu changamoto zinazoikabili jamii.
“Tunatoa wito kwa viongozi wa shule na bodi kuhakikisha vifaa hivi vinatunzwa ili viweze kuwasaidia wanafunzi wa sasa na wa vizazi vijavyo,” alisema Mkude.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa, alisema msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Aliwataka walimu kuunda kamati maalum za kusimamia usalama wa vifaa vya shule, huku akisisitiza kuwa wazazi wa wanafunzi watakaobainika kuharibu viti na meza kwa makusudi wawajibishwe.
“Kuanzia sasa, wazazi wa watoto wanaoharibu miundombinu ya shule waandikiwe barua na walipe fidia. Hatua hii itasaidia kupunguza upungufu wa vifaa kila mwaka,” alisema Mkalipa.
Msaada huu ni sehemu ya jitihada za NMB kuchochea maendeleo ya elimu nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya kujifunzia, na ni uthibitisho wa dhamira ya benki hiyo kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika kila kona ya Tanzania
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...