Na: Dk. Reubeni Lumbagala.


Kila ifikapo Tarehe 01 Mei ya kila mwaka, huadhimishwa Siku ya Wafanyakazi Duniani. Kila nchi huadhimisha siku hii kwa utaratibu wake, muhimu ni kufanya tafakuri ya hoja za wafanyakazi ili hoja hizo zifike katika mamlaka husika ziweze kutatuliwa kwa ustawi wa wafanyakazi na maendeleo ya nchi.

Hapa nchini, kwa mwaka huu wa 2025, maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kitaifa yamefanyika mkoani Singida huku Mgeni Rasmi akiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Kwa upande wa maadhimisho ngazi ya mikoa, kila mkoa umeadhimisha kwa namna yake. Maadhimisho hayo yamechangizwa na kaulimbiu isemayo "Uchaguzi Mkuu wa 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali na Kuthamini Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki."

Kwa kuzingatia tukio kubwa na la muhimu katika nchi yetu kwa mwaka huu 2025 yaani uchaguzi mkuu, viongozi wa vyama vya wafanyakazi pamoja na wanachama wao kwa ujumla, wameridhia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kwa mwaka huu, kuwe na kaulimbiu yenye kuchagiza wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu kwani ni katika ushiriki wao ndipo viongozi bora na maendeleo ya kweli yanapatikana. Kwahiyo, katika maadhimisho hayo, wito umetolewa kwa wananchi wenye sifa stahiki, washiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Kimsingi, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kote duniani, wafanyakazi huandaa hotuba yenye kubeba mafanikio na changamoto zinazowakabili ili mamlaka husika ziweze kufanyia kazi. Kwa upande wa changamoto, hoja ya nyongeza ya mshahara imekuwa ndiyo hoja kinara, kutokana na umuhimu wake katika kujenga ustawi wa wafanyakazi na kuchagiza maendeleo pia. Hivyo basi, macho na masikio ya wafanyakazi katika maadhimisho ya Mei Mosi yanaangazia zaidi kwenye nyongeza ya mishahara. Huu ndiyo ukweli bila kupepesa macho.



Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeendelea kupaza sauti yake kwa serikali kuhusiana na nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi ili kuwawezesha wafanyakazi kumudu gharama za maisha na kuboresha utumishi wa umma. Ni jambo la faraja kuona, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesikiliza kilio cha wafanyakazi kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1, hivyo kufanya kima cha chini kupanda kutoka shilingi 370,000 hadi 500,000, huku utekelezaji wake ukitarajiwa kuanza rasmi Tarehe 01 Julai, 2025 katika mwaka mpya wa fedha 2025/2026.

"Kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa, mimi na wenzangu, baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda, ninayo furaha kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu, serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1," amesema Rais Dk. Samia. Sambamba na hilo, wafanyakazi wa ngazi nyingine za mishahara, Rais Dk. Samia ameahidi kuwaongezea mshahara pia.

Kwahiyo, wafanyakazi wote wameguswa na nyongeza hii kwa namna mbalimbali. Ikumbukwe, nyongeza ya mshahara inawapa unafuu wafanyakazi kwani kiasi kinachoongezeka hutumika katika kuboresha maisha yao, ndiyo maana kilio cha nyongeza ya mishahara huwa kikubwa kutokana na umuhimu wake huu, lakini kubwa nyongeza ya mishahara ni muhimu ili kuendana na gharama za maisha.

Nina kila sababu ya kuungana na wananchi wenzangu, kumpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwajali wafanyakazi kwa kuongeza kima cha chini ya mshahara na kuwaongezea mishahara wafanyakazi wa ngazi nyingine za mishahara. Katika kuitendea haki dhana ya haki na wajibu, serikali imetimiza wajibu wake wa kujali maslahi ya wafanyakazi, kwa upande wa wafanyakazi nao wana jukumu la kufanya kazi kwa juhudi na maarifa makubwa ili kuongeza tija na uzalishaji nchini kwa maendeleo endelevu. Labda tu Rais wangu Dk. Samia nikutie moyo kuwa, hili la nyongeza ya mshahara umethibitisha pasi na shaka kuwa wewe ni rafiki wa wafanyakazi, na upo nao bega kwa bega.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Maoni: 0620 800 462.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...