Na John Mapepele

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati kuisogeza Serikali karibu zaidi na wananchi wake hasa wale walio na kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini ili kuwaletea maendeleo.

Akizungumza kwenye Kongamano la Uchumi la Arusha leo Mei 3, 2025 jijini Arusha akiwa miongoni mwa watoa mada, Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba lengo kuu ni kuwakomboa wananchi kutoka katika mnyororo wa ukosefu wa taarifa, huduma na fursa, kwa kuwajengea uelewa, uwezo na maarifa ya msingi, sambamba na kuwawekea miundombinu inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo.

“Tupo katika zama ambazo maendeleo hayategemei tena maamuzi ya viongozi wa kitaifa peke yao, bali yanategemea uwezo wa maeneo yetu ya mikoa na halmashauri zetu kuongoza kwa dira, maarifa na maamuzi ya kimkakati”.Amefafanua Mhe. Mchengerwa 
Aidha, amesema utawala bora siyo tu matumizi ya sheria bali ni falsafa ya kuwezesha kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika ndoto ya taifa na kujenga taasisi imara, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na kutoa huduma kwa usawa bila upendeleo.

Amesisitiza kuwa kwa kutumia sera ya Decentralization by Devolution (D-by-D), halmashauri zimewezeshwa kupanga na kutekeleza mipango yao kulingana na vipaumbele vya wananchi wao na kwamba hiyo ndio njia ya kweli ya kukuza demokrasia ya kiuchumi.

”Kwa maana hiyo, TAMISEMI imewapa halmashauri zetu nguvu ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa mazingira ya jamii zao. Hili linawezesha uwekezaji wa ardhi, huduma bora kwa wananchi, na kuimarisha mapato ya ndani”. Ameongeza Waziri Mchengerwa 

Akifafanua zaidi amesema ustawi wa mikoa hautatokana na maazimio ya makaratasi pekee, bali na uthubutu wa viongozi wake kuondoa matabaka baina ya walionacho na wasio nacho ambapo amesisitiza mikoa ina wajibu wa kufanya tafiti za kina za fursa zilizopo, kutambua changamoto kisekta, kutafuta majawabu yanayotekelezeka na kuanzisha ubia mtambuka (multi-sectoral partnerships) kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Waziri Mchengerwa ameagiza kwamba kongamano lisiwe tu mkutano wa mijadala, bali chemchemi ya fikra mpya, dira ya uwekezaji wenye tija, na mlango wa fursa kwa kila raia wa Mkoa wa Arusha iwe ni kijijini au mijini.

Ametaka ongamano hilo liwe chachu ya kufungua milango mipya ya uwekezaji kwa kushirikisha Wizara na Taasisi zote husika za Serikali ili kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yanaboreshwa kwa wepesi, uwazi na ushawishi chanya.

Maeneo yaliyotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya uwekezaji yaharakishwe kuhuishwa kwa kupangwa kitaalamu, kupimwa kwa usahihi, fidia zote itolewe kwa haki, na miundombinu ya msingi (barabara, maji, umeme, mawasiliano na huduma nyingine) ijengwe kwa haraka.
Amesisitiza kuwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali washirikishwe kwa kina, kwa uwazi, na kwa heshima pasipo ubaguzi wa hali za kiuchumi, jinsia, mila wala hadhi ya mtu.

Pia mchango wa wananchi wa kawaida unaojumuisha wakulima, wafanyabiashara wadogo, vijana na wanawake lazima uwekwe kikamilifu kwenye mpango unaotokana na Kongamano hili.

Aidha, ameelekeza sheria za nchi zisimamiwe kwa haki, weledi na uadilifu ili kulinda rasilimali za Mkoa na taifa na kwamba tusiruhusu migogoro isiyo ya lazima ififishe ndoto za mamilioni bali, tutumie maarifa ya ndani na teknolojia ya kisasa, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa ndani na nje ya nchi, ili kubuni uwekezaji wa kisasa wenye tija na ustahimilivu wa muda mrefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...