Na Mwandishi Wetu – Songea

Sekta ya kilimo mkoani Ruvuma imeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa huo, baaday ya kuonyesha ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao ya biashara, hususan tumbaku, ufuta, mbaazi na soya, katika msimu wa mwaka 2024/2025.

Takwimu zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la tumbaku umeongezeka kutoka tani 1,664 kwa msimu wa mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 2,053 msimu wa 2024/2025, aidha uzalishaji wa zao la ufuta umefikia tani 5,538 msimu huu, na matarajio ni kuvuka tani 10,000 ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026.

Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji madhubuti wa mfumo wa stakabadhi gharani, ambao umewezesha wakulima kupata bei nzuri na uhakika wa soko, mfumo huo pia umeongeza uwazi katika biashara ya mazao na kuchochea ushirikiano baina ya wakulima, vyama vya msingi na wanunuzi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa kawaida wa 22 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao Songea Namtumbo (SONAMCU), Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, amesema mafanikio hayo ni ushahidi kuwa kilimo kinaendelea kuchochea uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kwani SONAMCU inasaidia kuongeza pato la Mkoa na Taifa kwa ujumla.

“Chama Kikuu cha SONAMCU kinatoa mchango mkubwa katika kukuza pato la Mkoa na uchumi wa Taifa kupitia usimamizi wa uzalishaji na masoko ya mazao ya biashara. Tunataka chama hiki kiwe mfano wa kuigwa,” alisema Makondo.

Aidha, metangaza kuwa msimu mpya wa minada ya ufuta utaanza rasmi Mei 29, 2025 katika Wilaya ya Namtumbo, hatua inayotarajiwa kuwaletea wakulima mapato zaidi kutokana na ongezeko la bei ya zao hilo katika soko.

Kwa upande wake, Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga, amesema kuwa jukumu la chama hicho ni kuratibu na kusimamia masoko ya zao la Tumbaku pamoja na mazao yanayopitia mfumo wa stakabadhi gharani ambayo ni ufuta, soya na Mbaazi pamoja na kutoa elimu ya kilimo cha biashara kwa wakulima wake.

Naye mkulima kutoka Wilaya ya Namtumbo, Eleterius Cosmas Mbawala, alieleza kuwa hali ya kilimo kwa sasa ni ya kuridhisha, kutokana na msaada unaotolewa na vyama vya msingi kwa wakulima ikiwemo ushauri wa kitaalamu na pembejeo Hata hivyo, ametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa bidhaa za wakulima zinauzwa kwa kutumia shilingi ya Tanzania na kulipwa kwa shilingi badala ya dola ili kuondoa mkanganyiko kwa wakulima wanaoshindwa kuelewa thamani ya dola.

Chama Kikuu cha Ushirika SONAMCU, kilichoanzishwa mwaka 2003 chini ya Sheria ya Ushirika Na. 15 ya mwaka 1991, kinaundwa na vyama vya msingi 50 kutoka halmashauri tano za Mkoa wa Ruvuma, kikiendelea kuwa kiunganishi muhimu kati ya wakulima na soko la uhakika.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi wa vijijini, mafanikio ya SONAMCU yanadhihirisha jinsi ushirika unavyoweza kuwa chombo cha mabadiliko ya kiuchumi ikiwa utasimamiwa vizuri, na kuungwa mkono na wakulima.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...