Na. Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zimetia Saini mikataba miwili ya msaada wa jumla ya Yuan za China milioni 500, sawa na shilingi bilioni 185 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na kusaidia program ya ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu.
Mikataba hiyo imesainiwa Ofisi za Wizara ya Fedha (Treasury Square) na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Dkt. Nchemba, alisema kuwa Mkataba wa kwanza ni wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kitaalam wenye thamani ya Yuan za China milioni 200 sawa na shilingi bilioni 74.2 na Mkataba wa pili kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha matibabu na upasuaji wa moyo Afrika Mashariki na Kati wenye thamani ya Yuan za China milioni 300, sawa na shilingi bilioni 111.2.
“Lengo la misaada hii ni kuwezesha utekelezaji wa miradi itakayochaguliwa na kukubalika kwa pamoja na Serikali za Tanzania na China, na mkataba wa pili una lengo la kujenga Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Magonjwa ya Moyo ya Watoto kwa ajili ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati”, alieleza Dkt. Nchemba.
.
Dkt. Nchemba alisema kuwa, msaada wa Ushirikiano wa kiuchumi na Kitaalamu ni ahadi aliyoitoa Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, wakati wa kikao chake na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tisa la Kilele la Ushirikiano wa China na Afrika la mwaka 2024, uliofanyika jijini Beijing.
Alisema kuwa msaada wa ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo kwa watoto Mloganzila - unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kama vile upatikanaji wa huduma bora za afya, kukuza uchumi kupitia kuongeza ajira na kuchochea biashara kwa wananchi ili kuboresha maisha yao, kukuza utafiti katika masuala ya afya na elimu na kuendeleza miundombinu.
Alisema kuwa misaada hiyo inadhihirisha kwamba Jamhuri ya Watu wa China inabaki kuwa rafiki wa kweli na wa kutumainiwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na kuendelea kudumisha urafiki wa muda mrefu kwa manufaa ya pande hizo mbili.
Aidha amemhakikishia Balozi huyo wa China utayari wa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya China.
Kwa upande wa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe.Chen Mingjian, alisema kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kutokana na ushirikiano wa kihistoria wa muda mrefu na pia imani ya Tanzania kwa nchi hiyo katika kukuza maendeleo ya wananchi.
Aidha alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi kinara yenye ushirikiano bora wa kiuchumi na kijamii na imeshirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, mradi ambao umekuwa wa kielelezo cha uhusiano huo.
Alisema kuwa msaada wa sekta ya afya kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambao umelenga kunusuru maisha ya watoto wanaougua maradhi ya moyo, pia utakuza ajira na kuwa sehemu ya utalii wa kimatibabu watakaokuja nchini kutoka mataifa mengine.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge, aliishukuru China kwa ufadhili huo utakao kuwa mkombozi mkubwa wa matibabu ya moyo kwa watoto kupitia ujenzi wa Kituo hicho cha Umahiri kitakachojengwa katika Hospitali ya Mloganzila.
Alisema kuwa changamoto ya kiafya kwa watoto inayosababishwa na maradhi ya moyo ni kubwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya Watoto 200 wanaozaliwa, Watoto wawili wanazaliwa wakiwa na matatizo ya moyo na kwamba ujenzi wa Kituo hicho cha umahiri utaondoa changamoto ya matibabu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mhe. Ismail Rumatila, ambaye aliahidi kuwa Serikali itasimamia utekelezaji wa mradi huo kama ilivyokusudiwa ili kuleta tija na kuboresha upatikanaji wa huduma na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Che Mingjian, wakitia saini Mikataba miwili ya msaada wa jumla ya Yuan za China milioni 500, sawa na shilingi bilioni 185 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha magonjwa ya moyo pamoja na mradi wa ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu, hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Che Mingjian, wakibadilishana wakitia saini Mikataba miwili ya msaada wa jumla ya Yuan za China milioni 500, sawa na shilingi bilioni 185 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha magonjwa ya moyo pamoja na mradi wa ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu, hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Che Mingjian, wakionesha wakitia saini Mikataba miwili ya msaada wa jumla ya Yuan za China milioni 500, sawa na shilingi bilioni 185 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha magonjwa ya moyo pamoja na mradi wa ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu, hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...