· Siku ya Ulaya 2025 yaadhimisha Miaka 50 ya ushirikiano wa EU na Tanzania na Miaka 25 ya mahusiano ya EU na AU

· Miongoni mwa wageni rasmi walikuwepo, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), maafisa waandamizi wa serikali, asasi za kiraia, wanahabari, vijana na wanadiplomasia.

· Nishati imekuwa kiini cha maadhimisho ya mwaka huu, ambapo Timu ya Ulaya imejitolea zaidi ya TZS trilioni 3 kwa sekta ya nishati Tanzania kupitia Mpango wa Global Gateway.

Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa EU leo wameadhimisha Siku ya Ulaya 2025, wakikumbuka miaka 50 ya ushirikiano kati ya EU na Tanzania, na miaka 25 ya mahusiano kati ya EU na Umoja wa Afrika. Tukio hili limeonesha ushirikiano wa kimkakati unaoimarika kati ya EU na Tanzania.

Maadhimisho ya mwaka huu yamejikita katika Nishati Mbadala na msaada wa EU kwenye eneo hili. Upatikanaji wa nishati safi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya Tanzania, ukuaji wa uchumi na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Hafla hiyo imewakutanisha Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, mabalozi wa EU, maafisa wa serikali, vijana, wanahabari, wanadiplomasia

Katika hotuba yake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Mheshimiwa Christine Grau, alisisitiza kwa undani ushirikiano wa EU na Tanzania:

"Ushirikiano wetu unazidi kuwa wa kimkakati, ukijengwa juu ya maslahi ya pamoja na ustawi wa pande zote. Sisi si wafadhili tu – sisi ni washirika wa kweli. Kupitia mkakati wa Global Gateway, tunaunga mkono jitihada za Tanzania katika nishati mbadala, kidigitali, uongezaji thamani na miundombinu endelevu."

Mhe. Kombo alikaribisha msaada endelevu wa Umoja wa Ulaya, hasa katika sekta ya nishati, na kupongeza EU kwa kuoanisha ushirikiano wake na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Kupitia mkakati wa Global Gateway, Timu ya Ulaya imeahidi EUR milioni 990 (zaidi ya TZS trilioni 3) kusaidia sekta ya nishati ya Tanzania. Hii ni pamoja na mchango wa moja kwa moja wa EUR milioni 191.9 (TZS bilioni 565) kutoka EU kwa ajili ya nishati safi na kuunganisha nishati za mpakani. Miradi mikubwa ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono (EUR milioni 299, TZS bilioni 880), ambapo EU inachangia EUR milioni 36 (TZS bilioni 106), pamoja na ushiriki katika miradi ya miunganisho ya nishati na Zambia na Uganda yenye thamani ya EUR milioni 604.4 (TZS trilioni 1.8).

EU pia inaunga mkono matumizi ya majiko safi kwa uwekezaji wa sasa wa EUR milioni 30 (TZS bilioni 88) na mpango mpya wa kikanda wa EUR milioni 20 (TZS bilioni 59) ili kuongeza suluhisho za nishati safi. Uwekezaji zaidi katika miundombinu ya nishati kwa sekta za kilimo na madini uko mbioni.

Ushirikiano huu hauishii kwenye miundombinu pekee. Wageni wa Siku ya Ulaya walikutana na wanawake vijana wa Kitanzania wanaosomea fani za nishati – walionufaika na ufadhili wa masomo kutoka EU, UNDP na Ubalozi wa Ireland. Novemba 2024, ufadhili wa masomo 25 ulitolewa katika uhandisi wa nishati endelevu, na kufanya idadi kufikia 35. Mpango huu, uliopo katika Mpango wa Kwanza wa Tanzania wa Ufanisi wa Nishati, unalenga usawa wa kijinsia katika sayansi na teknolojia na kusaidia mabadiliko jumuishi kuelekea uchumi wa kijani.

Balozi Grau aliongeza kuwa katika miaka saba iliyopita, msaada wa EU wa EUR milioni 65 (TZS bilioni 192) umewezesha vijiji zaidi ya theluthi moja Tanzania kuunganishwa na umeme, na kuboresha upatikanaji wa nishati kwa zaidi ya watu milioni moja vijijini. EU inajiandaa kuanza awamu mpya ya ushirikiano mwaka 2026, unaoendana na Dira ya 2050, ukiweka mkazo kwenye ustahimilivu wa tabianchi, ukuaji endelevu, ajira kwa vijana, na utawala bora wa kidemokrasia. EU itaendelea kuwa mshirika mkuu wa Tanzania katika biashara, uwekezaji na maendeleo, ikizingazia amani, ustawi na maendeleo jumuishi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...