Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2025/26 imewasilishwa rasmi bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo pamoja na taasisi zilizo chini yake kama vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

 

Mara baada ya kuwasilishwa, wadau mbalimbali wa maendeleo na masuala ya kijamii wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu bajeti hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kujumuisha mahitaji ya makundi yote ya kijamii, hususan wanawake na vijana.

 

Ocheki Msuva, Mkurugenzi wa Shirika la Bridge for Change, ni miongoni mwa wadau waliopitia bajeti hiyo kwa karibu. Akitoa maoni yake, Bw. Msuva amesema bado kuna changamoto ya ujumuishaji wa jinsia, ambapo miradi mingi ya uwekezaji huonekana kuwanufaisha zaidi wanaume.

 

"Kuna haja ya kupitia upya Dira ya Taifa ili miradi ya uwekezaji tunayoiweka iguse makundi yote ya kijamii. Ajira nyingi zinazotokana na miradi hiyo zinaelekezwa kwa wanaume, hali inayowatenga wanawake katika maendeleo ya taifa lao," amesema Bw. Msuva.

 

Naye mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, Kenneth Anjelita, ameitaka serikali kuhakikisha kuwa bajeti zake zina uhalisia unaoweza kuonekana moja kwa moja katika maisha ya wananchi wa kawaida.

 

"Bajeti inapaswa kuwa chombo halisi cha maendeleo. Wananchi wanataka kuona mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku. Hii ni pamoja na huduma bora za afya, hasa kwa wanawake na watoto walioko maeneo ya vijijini ambako huduma hizo bado ni changamoto," amesema Kenneth.

 

Wadau hao wametoa rai kwa serikali kuendelea kusikiliza maoni ya wananchi wakati wa mchakato wa kuandaa na kutekeleza bajeti. Wamesisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa ufanisi ndio kipimo halisi cha mafanikio ya mipango ya maendeleo ya taifa.

 

Kwa ujumla, bajeti ya 2025/26 imeonekana kuwa na malengo makubwa ya kukuza uwekezaji nchini, lakini wadau wanashauri kuwa mafanikio yake yatategemea namna ambavyo itatekelezwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...