Wakala wa Vipimo Tanzania wamepokea na kusimika mtambo mpya wa kisasa wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400, kwa ajili ya kuhakikisha dira za maji. Mtambo huo una uwezo wa kupima hadi dira 1,000 kwa siku, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na usahihi katika uhakiki wa mita za maji nchini.

 

Kupitia maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani, Wakala wa Vipimo wameendesha zoezi la kutoa elimu kwa wananchi pamoja na madereva wa malori katika kituo chao kilichopo Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani. Elimu hiyo ililenga kuwaeleza wananchi umuhimu wa uhakiki wa dira za maji pamoja na faida zake katika matumizi ya kila siku ya maji majumbani na kwenye taasisi mbalimbali.

 

Akizungumza katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala wa Vipimo, Bw. Karim Mkorehe, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia mtambo huo mpya wenye uwezo mkubwa wa kuhakiki dira za maji.

 

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo katika Kituo cha Misugusugu, Bw. Gaudence Gaspary, alisema kuwa elimu hiyo imetolewa kwa makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo madereva wanaopata huduma katika kituo hicho. Alifafanua kuwa dira ya maji inapaswa kuhakikiwa angalau mara moja kwa mwaka ili kuhakikisha usahihi wa gharama za matumizi ya maji.

 

Aidha, baadhi ya wananchi waliopatiwa elimu hiyo walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo huku wakikiri kuwa wengi wao hawakuwa na uelewa juu ya uwepo wa huduma za uhakiki wa mita za maji.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...