▪️Yatoa hati za makosa kwa kukiuka masharti ya Leseni

▪️Kampuni 7 tu kati ya 95 ambazo hazijaanza uchimbaji zimelaza mtaji wa Trilion 15 

▪️Zapewa siku 30 kujibu hoja

SERIKALI  imetoa Hati za Makosa kwa Kampuni  95 za Uchimbaji Mkubwa na wa Kati wa Madini kutokana na wamiliki wa leseni hizo kukiuka masharti ya Leseni  kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Madini.

Akizungumza leo Mei 6, 2025 jijiini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kampuni hizo zinapaswa kujibu hoja ndani ya siku 30 la sivyo zitafutiwa leseni zao.

Hati hizo za makosa zimetolewa rasmi kuanzia Aprili 14, 2025 na muda wake utamalizika Mei 13 mwaka huu. 

 “Kama wanahoja walete majibu yao, tuyahakiki tukijiridhisha na hoja zao tutawaondolea makatazo kama hawana hoja tutawafutia leseni zao kwa  mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123  ya  utoaji na ufutaji wa leseni za  madini na uchimbaji kifungu cha 63 na Kanuni zake, ambacho kinaeleza ukipewa leseni unapaswa uanze kazi ndani ya miezi 18.

Amesema, Serikali imetoa leseni kwa wachimbaji wa kati na wakubwa ambazo tangu kutolewa kwake hazifanyiwa kazi.

Zipo Kampuni tangu zimechukua leseni mwaka 2011 mpaka leo hazijaingiza hata koleo kwenye eneo miaka 14 sasa hazijaanza shughuli zozote, hatuwezi kuwa nchi ya namna hii.

Leseni 7 tu kati ya 95 ukiziweka pembeni zina mtaji wa Shilingi Trilioni 15 zimelala, sisi hatuwezi kuwa nchi ambayo  inatoa leseni kwa ajili ya kuchochea sekta ya madini kukua,halafu kuna watu wanachukua leseni wanakaa nazo hawafanyii kazi kwa kisingizio kuwa tupo kwenye mazungumzo na serikali  na sababu mbali mbali.

Leseni za madini zikitolewa zina masharti nyuma yake kwenye ile karatasi hakuna sharti linalosema mtu  ataanza uchimbaji wa madini nchini Tanzania akikamilisha mazungumzo na serikali, hiyo si sehemu ya sharti.

Masharti ni kwamba mwombaji anapopewa  leseni ni lazima aanze uchimbaji ndani ya miezi 18 vinginevyo awe na sababu ambazo zimeridhiwa na Waziri wa Madini kupitia Tume ya Madini, vinginevyo unapaswa kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18.

Amesema na wale wote ambao  wamepata hati  ya makosa ambao wamejibu waende na barua ya ‘Commitment’ ya kueleza wataanza uchimbaji lini, ambao katika barua hiyo pia ikitokea ameshindwa kukidhi kile alichosema kwenye barua  sheria itafuata mkondo wake.

Kuna vitu kama nchi ni lazima tuchukue maamuzi magumu, hatuwezi kuifanya nchi yetu mtu anakuja anachukua leseni alafu akaitafutie mtaji, sheria inataka mtu yoyote anayekuja kufanya maombi ya leseni lazima atoe udhibitisho wa uwezo wa kifedha na kiufundi kabla ya kupata leseni,  sio nikupe ndio ukatafutie mtaji maana yake utakuwa umekiuka masharti ya sheri kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi wakati wa kuomba leseni.

Wale wote ambao hawatajibu ndani ya muda uliowekwa wasitegemee huruma yoyote, na wamekuwa ni mabingwa wakukimbilia mahakamani kuishtaki serikali katika hili Serikali imefuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria inayowataka waliopata Leseni wote kufanya uendelezaji wa Leseni zao” Alisema Mavunde

Sekta ya Madini ni kati ya sekta zenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo shughuli za uchimbaji wa madini huchochea maendeleo makubwa ya kiuchumi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...