Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameiagiza Bodi ya Usajili
wa Wahandisi (ERB) kuongeza juhudi za kusajili wataalam wa kada ya mafundi
sanifu na kuwajengea uwezo, kwani idadi iliyopo sasa hailingani na ile
wanaostahili kusajiliwa.
Waziri Ulega alitoa agizo hilo leo tarehe 22 Mei, 2025
mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya saba ya siku ya mafundi sanifu
ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mafundi sanifu zaidi ya 800
ukiwa na mada isemayo ‘Muundo wa utumishi kwa kada ya mafundi sanifu katika
utumishi wa umma na sekta binafsi’.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Waziri Ulega pia
aliiagiza bodi hiyo ishirikiane na vyuo vinavyozalisha wataalam hao ili
kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wanaosomea fani hizo.
Vilevile, Waziri Ulega aliiagiza Bodi ya Usajili wa
Wahandisi (ERB) kuongeza idadi ya usajili wa mafundi sanifu wa uhandisi wenye
sifa stahiki za kitaaluma na ambao wana uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la
ajira na katika miradi ya kimkakati hapa nchini.
Kadhalika, Waziri Ulega alisema katika jitihada za kukuza
uchumi Serikali itaendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kibiashara na
ya uwekezaji katika viwanda pamoja na kuhamasisha wadau kujenga viwanda vipya
hususan vile vinavyotumia malighafi za ndani.
Hivyo, aliwataka mafundi sanifu hao kuchapa kazi, kufanya
kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa pamoja na kukamilisha miradi yote vizuri kwa
muda uliopangwa na kwa thamani iliyo halisi.
Waziri Ulega alisema Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na
bodi za kitaaluma ikiwemo ERB na AQRB wameanza zoezi la kupitia upya muundo wa
utumishi na maslahi ya wataalam wa ujenzi.
Alisema Serikali inafahamu changamoto wanazopita mafundi
sanifu pamoja na kupanda vyeo kwa njia ya mserereko hususani fundi sanifu
aliyefikia cheo cha afisa mkuu akiwa mhandisi asianze mwanzo.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mwajuma Waziri aliwataka
mafundi sanifu kushikamana kwa upendo ili waweze kutimiza malengo yao
waliyoyaweka.
Alisema mafundi sanifu ni kada muhimu inayotegemewa katika kuhakikisha michoro ya miradi inatekelezeka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...